Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya nguzo hizi sita ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ

“Si wema pekee kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi, lakini wema wa kweli kabisa ni mwenye kuamini Allaah na siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii.”[1]

MAELEZO

Wakati Shaykh alipotaja nguzo hizi akataja dalili yake kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Kwa sababu kitu chochote katika mambo ya dini, mambo ya ´ibaadah, mambo ya ´Aqiydah na mambo ya hukumu za Kishari´ah kinahitajia dalili. Kisipokuwa na dalili basi hakiwi sahihi. Pindi Shaykh alipotaja nguzo za imani akataja dalili yake kutoka katika Qur-aan kwanza kisha kutoka katika Sunnah. Kutoka katika Qur-aan ni maneno Yake (Ta´ala):

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ

“Si wema pekee kuelekeza nyuso zenu…”

Wema ni kitendo cha kheri kinachokurubisha kwa Allaah na kumfikisha mtu katika Pepo Yake. Kila kitendo cha kheri ni katika wema. Wema ni tamko lililoenea ambalo limekusanya aina zote za kheri. Aina mbalimbali za utiifu ni zenye kuingia chini ya jina “wema” na chini ya jina “taqwa”. Wema na taqwa ni katika majina yenye kuenea ambayo yamekusanya sifa zote za kheri. Maneno Yake (Ta´ala):

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ

“Si wema pekee kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi… “

Hii ni Radd kwa mayahudi waliokemea kubadilishwa Qiblah kutoka Yerusalemu na kuelekea Ka´bah tukufu. Walikemea jambo hili na wakalipinga pamoja na kujua kwamba ndio haki. Lakini hata hivyo wakalipinga kwa sababu ya inda, kiburi na kumhusudu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na juu ya Ummah huu. Ndipo Allaah akasema sio wema pekee kuelekeza nyuso zenu upande wowote pasi na amri kutoka kwa Allaah. Lakini wema khaswa ni kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Akikuamrisheni jambo basi ni lazima kwenu kulitekeleza. Huu ndio wema. Akikuamrisheni kuelekea Yerusalemu basi wema katika wakati huo ni nyinyi kuelekea Yerusalemu. Kwa sababu ndio kumtii Allaah (´Azza wa Jall). Kisha akikuamrisheni kuelekea Ka´bah wema ni nyinyi kuielekea Ka´bah. Kwa hiyo wema unazunguka pamoja na amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Nyinyi ni waja ambao mnatakiwa kutekeleza. Allaah akikuamriheni kuelekea upande fulani basi ni lazima kwetu kutekeleza. Ama kufanya kasumba ya upande fulani na kusema kuwa hakuna upande wenye kusihi isipokuwa upande fulani pekee hiyo maana yake ni kufuata matamanio na ushabiki. Mja wa kweli ni yule mwenye kuzunguka pamoja na maamrisho ya Allaah kule yalikoelekea. Hapingani na maamrisho ya Allaah. Kwa sababu kuelekea upande fulani baada ya kufutiwa sio kumtii Allaah (´Azza wa Jall). Kutendea kazi kitu kilichofutwa na kuacha kile kilichokuja kufuta sio kumtii Allaah. Huku ni kutii matamanio na ushabiki. Wema umefungamana na kumtii Allaah. Elekea popote ulipoelekezwa ikiwa kweli wewe ni mwenye kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall):

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ

“Si wema pekee kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi, lakini wema wa kweli kabisa ni mwenye kuamini Allaah na siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii.”[2]

[1] 02:117

[2] 02:117

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 219-221
  • Imechapishwa: 26/01/2021