Hadiyth hii inathibitisha kwamba ikiwa mwezi mwandamo haukuonekana usiku wa siku ya thelathini kwa mawingu au vumbi, basi inapaswa kukamilisha idadi ya Sha´baan kuwa siku thelathini na watu wasifunge usiku huo na hivyo inakuwa maana ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”… basi ikadirieni… “

ni kuikadiria idadi ya mwezi. Kwa msemo mwingine Sha´baan ikamilishwe kuwa siku thelathini, kama ilivyotangulia katika Hadiyth ya Abu Hurayrah:

”Mkifunikwa na mawingu, basi mkamilishe idadi ya Sha´baan siku thelathini.”

Hii ni dalili ya wazi isiyokubali tafsiri nyingine.

Kundi la wanazuoni wa madhehebu ya Hanaabilah wameona kuwa ni wajibu kufunga siku ya thelathini ikiwa mwezi mwandamo hautoonekana kutokana mawingu au vumbi kwa kushika tahadhari[1]. Wamesema maana ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”… basi ikadirieni… “

kwamba ibaneni idadi yake. Kama alivosema Allaah (Ta´ala):

وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ

“… na yule aliyebaniwa riziki yake… ”

Kwa maana ya kwamba riziki yake imebana. Kubana maana yake ni kwamba Sha´baana itafanywa kuwa siku ishirini na tisa. Wamesema kwamba Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amefafanua Hadiyth hii kwa matendo yake, yeye ndiye mpokezi wake na anajua zaidi maana yake. Naafiy’ amesimulia:

”´Abdullaah alikuwa Sha´baan inapomaliza siku ishirini na tisa, basi anamwagiza mtu atazame. Ikiwa utaonekana ni vyema. Na ikiwa haukuonekana na hakuna mawingu au vumbi, basi anafungua. Na ikiwa atazuiwa na mawingu au vumbi, basi anaamka amefunga.”[2]

Maoni ya kwanza ndio sahihi; kwamba ni lazima kula siku ya thelathini ikiwa utajificha mwezi kutokana na mawingu au vumbi kwa sababu ya yaliyotangulia. Kufasiri ya Hadiyth kwa Hadiyth ni jambo linapewa kipaumbele. Kuhusu matendo ya Ibn ´Umar yanapingana na dalili. Maneno ya Swahabah yanapopingana na maandiko yanakataliwa. Ni jitihaad yake ambayo inaweza kupatia na kukosea. Tafsiri ya mwekaji Shari´ah na maelezo yake yanatangulizwa mbele ya tafsiri ya mwingine. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alikuwa na matendo aliyotofautiana nayo peke yake, kama alivyoeleza  hayo Ibn-u-Qayyim na wengine – na Allah ndiye mjuzi zaidi.

[1] Tazama ”al-Mughniy” (03/330) na “al-Inswaaf” (03/269).

[2] Ziada hii iko kwa Abu Daawuud (2320) na Ahmad (8/71). Cheni ya wapokezi wa Hadiyth ni Swahiyh.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/13)
  • Imechapishwa: 30/01/2025