Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na sharti zake ni kumi:

1 –  Uislamu.

2 – Kuwa na akili.

3 – Kuweza kupambanua.

4 – Nia.

5 – Mtu asinuie kuukata [wudhuu´ wake] mpaka atakapomaliza kutawadha.

6 – Kukatika kwa yale yanayowajibisha wudhuu´.

7 – Kujisafisha kwa maji au kwa kutumia mawe kabla yake.

8 – Maji yawe masafi na yenye kuruhusiwa/ya halali.

09 – Kuondosha kila kinachozuia maji kufika kwenye ngozi.

10 – Kuingia kwa wakati wa kile kitendo cha faradhi kwa yule ambaye daima yuko katika hali ya hadathi.

MAELEZO

Maneno yake mtunzi:

“Sharti… “

Sharti za wudhuu´ ni kumi. Mtunzi (Rahimahu Allaah) anazungumzia sharti za kusihi kwa swalah ambapo (Rahimahu Allaah) akataja sharti za wudhuu´. Kwa sababu kuondosha hadathi – nako ni kule kutawadha – ni moja miongoni mwa sharti za kusihi kwa swalah. Wudhuu´ hausihi isipokuwa kwa sharti kumi ambazo ni lazima zitangulizwe ili wudhuu´ uwe wenye kusihi.

1 – Uislamu

Tayari tumeshatangulia kutaja maana ya Uislamu kwamba ni kujisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujiepusha na shirki na washirikina. Kwa msemo mwingine ni lazima mtawadhaji awe muislamu. Kafiri akitawadha hausihi. Kwa sababu kafiri hayakubaliwi wala hayasihi kutoka kwake matendo yoyote mpaka yajengeke juu ya Tawhiyd.

2 – Akili

Sharti ya pili miongoni mwa sharti za kusihi kwa wudhuu´ ni akili. Endapo atatawadha mwendawazimu, mtumzima ambaye kishachaganyikiwa au mtu aliyelazwa katika koma/icu wudhuu´ hausihi. Kwa sababu hana manuizi.

3 – Kuweza kupambanua

Sharti ya tatu miongoni mwa sharti za kusihi kwa wudhuu´ ni uwezo wa kupambanua. Endapo mtoto wa miaka mitano atamuona baba yake anatawadha ambapo na yeye akachukua maji na kupandisha puani, akasukutua, akaosha uso wake, mikono yake, akafuta kichwa chake na akaosha miguu yake akimwigiliza baba yake, wudhuu´ wake hausihi. Kwa sababu hajakuwa na uwezo wa kupambanua. Miaka ya kuweza kupambanua ni saba.

4 – Nia

Sharti ya nne miongoni mwa sharti za kusihi kwa wudhuu´ ni nia. Bi maana anuie kuondosha hadathi. Endapo mtu atapandisha maji puani, akasukutua, akaosha uso wake, mkono wake wa kuliani kisha wa kushotoni, akafuta kichwa chake kukiwemo masikio na pia akaosha miguu yake huku akikusudia kujitia baridi peke yake na asinuie kutawadha, haisihi. Kwa sababu hakunuia kutawadha.

Nia ni sharti katika ´ibaadah zote. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea katika “as-Swahiyh” zao kupitia kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakika si venginevyo kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kwa kile alichonuia.”[1]

Wudhuu´ hausihi pasi na manuizi, swalah, funga na wala zakaah isipokuwa kwayo. Nia inapambanua ´ibaadah hizi na zile. Wakati mwingine sura ya kitendo inakuwa moja na kitu pekee kinachopambanua kati yake ni nia. Kwa mfano wakati anapotoa mali kuwapa mafukara akinuia kuwa ni zakaah, basi inakuwa ni zakaah. Na akinuia kuwa ni swadaqah ya kujitolea, basi inakuwa ni swadaqah ya kujitolea. Na akinuia kuwa ni zawadi, basi  inakuwa ni zawadi. Wala hakuna haja ya kutamka nia kwa sauti.

5 – Mtu asinuie kuukata [wudhuu´ wake] mpaka atakapomaliza kutawadha

Sharti ya tano miongoni mwa sharti za kusihi kwa wudhuu´ ni mtu asinuie kuukata wudhuu´ wake mpaka atakapomaliza kutawadha. Endapo mtu atakata nia katikati ya kutawadha, basi hausihi. Bali ni lazima kueindeleza kuanzia mwanzo hadi mwisho wake. Asinuie kuikata mpaka atakapomaliza twahara yake.

[1] al-Bukhaariy (01) na Muslim (1907).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 19-22
  • Imechapishwa: 07/12/2021