10. Kuoga ndani ya bahari kunamtosheleza mtu na kutawadha?

Swali 10: Ikiwa karibu ya nyumbani kwangu kuna bahari au mto na nikawa naoga ndani yake na baada ya hapo ukafika wakati wa swalah na sina maji mengine ya kutawadha zaidi ya hayo.  Je, itafaa kwangu kuyatumia kama maji ya wudhuu´ au hapana[1]?

Jibu: Ni lazima kwako kutawadha kwa maji ya bahari au mto yaliyo karibu nawe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa juu ya kutawadha maji ya bahari ambapo akajibu kwa kusema:

“Maji yake ni masafi na maiti wake ni halali.”[2]

Haitoshi ikiwa umeoga kwa ajili ya kuondosha najisi au uchafu. Kwa sababu ni lazima kutawadha. Lakini kama umeoga kutokamana na janaba na ukanuia hadathi zote mbili – hadathi ndogo na hadathi kubwa – basi itatosha. Lakini bora ni kutawadha kisha ukaoga. Hivi ndivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya; akitamba kwanza, kisha anatawadha wudhuu´ wa swalah kisha anaoga. Hii ndio Sunnah. Lakini akinuia yote kwa nia moja kutamtosha kwa mujibu wa wanazuoni. Lakini bora kwa muislamu ni yeye kufanya yale aliyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vivyo hivyo mwanamke juu ya josho la hedhi na nifasi. Ni mamoja maji ni ya bahari, mto, visima au chemchem. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ

“Mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni na mkiwa wagonjwa au mko safarini au mmoja wenu akija kutoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi fanyeni Tayammum kwa ardhi kwa juu panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu.”[3]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/176-177).

[2] an-Nisaa´iy (59).

[3] 05:06

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 22/02/2022