10. Hukumu ya kumtukana Allaah na Mtume Wake kwa sababu za kimaisha

Swali 10: Ikiwa mtu atamtukana Allaah, atamtukana Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au akatukana dini, kisha akajitetea kwa kusema anatafuta riziki na maisha, anachokusudia ni kujipendekeza kama vile kusema:

“Nikimtukana Allaah, nitapata riziki na dunia.”

Jibu: Hapana shaka juu ya ukafiri wa mtu huyu. Kama ilivyotangulia mtu yeyote anayefanya kitendo cha ukafiri kwa makusudi na kwa khiyari yake basi anakufuru. Na mwenye kufanya kitendo cha ukafiri kwa mzaha, anakufuru. Na mwenye kufanya kitendo cha ukafiri kwa kuogopa, anakufuru. Na ikiwa atafanya kwa ajili ya kupata mali, basi huyu ni kafiri kwa mujibu wa dalili ya Aayah. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake [atapata adhabu] isipokuwa yule aliyetenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu ya iymaan. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu. Hivyo kwa sababu wao wamependelea uhai wa dunia kuliko wa Aakhirah.”[1]

Kwa hiyo Allaah ameeleza kwamba wao wana sehemu ya dunia na hivyo wakaipa kipaumbele dunia yao. Kwa hiyo Aayah ni dalili ya wazi kuhusu kundi hili la watu, kwamba wao wamefanya ukafiri kwa sababu ya kupendelea na kuipa dunia nafasi ya kwanza badala ya Aakhirah. Hivyo basi wanaingia ndani ya Aayah hii.

[1] 16:106-107

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah wa Ajwibah fiy-Iymaan wal-Kufr, uk. 29
  • Imechapishwa: 05/01/2026