10. Hadiyth “Baada ya kupita siku kumi na sita za Ramadhaan… “

1062- Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Baada ya kupita siku kumi na sita za Ramadhaan tulitoka kwenda vitani pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika sisi walikuweko waliofunga na wengine hawakufunga. Ambaye amefunga hakumtia kasoro ambaye hakufunga wala ambaye hakufunga hakumtia kasoro aliyefunga.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Walikuwa wakiona yule mwenye kuhisi nguvu akafunga basi  hivyo ndivo bora na wakiona kuwa yule mwenye kuhisi unyonge akala basi hivo ndivo bora.”

Ameipokea Muslim na wengine.

Wanachuoni wametofautiana ni kipi bora safarini, kufunga au kuacha kufunga? Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameonelea kuwa kufunga ndio bora zaidi. Hayo yamesimuliwa pia kutoka kwa ´Uthmaan bin Abiy-´Aasw. Maoni hayohayo ndio ameonelea Ibraahiym an-Nakha´iy, Sa´iyd bin Jubayr, ath-Thawriy, Abu Thawr na Hanafiyyah.

Maalik, al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw na ash-Shaafi´iy wamependelea zaidi kufunga kwa yule mwenye nguvu za kufanya hivo.

´Abdullaah bin ´Umar, ´Abdullaah bin ´Abbaas, Sa´iyd bin al-Musayyab, ash-Sha´biy, al-Awzaa´iy, Ahmad bin Hanbal na Ishaaq bin Raahuuyah wamependelea zaidi kuacha kufunga.

Imepokelewa kutoka kwa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz, Qataadah na Mujaahid wamependelea zaidi kile ambacho kitakuwa chepesi zaidi kwa mtu.  Haafidhw Abu Bakr bin al-Mundhir amechagua maoni haya. Ndio maoni mazuri na Allaah ndiye mjuzi zaidi[2].

[1] Nzuri.

[2] Yeye (Rahimahu Allaah) amesema kweli. Kilicho bora zaidi ni kile ambacho ni chepesi zaidi. Hali na hali za watu ni zenye kutofautiana. Kila mmoja achukue kile ambacho ni chepesi zaidi kwake. Kwa ajili hiyo imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema kumwambia mtu ambaye alimuuliza kuhusu kufunga safarini:

”Funga ukitaka na uache ukitaka.” (Muslim (3/145))

Katika upokezi mwingine Swahiyh imekuja:

”Fanya kile ambacho ni chepesi zaidi kwako.”

Imetajwa katika ”as-Swahiyhah” (2884).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/617-618)
  • Imechapishwa: 22/04/2020
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy