1. Ni wajibu kwa mwanamke kuufunika uso wake mbele ya wanaume ajinabi

Himdi zote ni za Allaah. Tunamhimidi na kumuomba msaada na msamaha. Tunajikinga Kwake kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna awezae kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa na Allaah, basi hakuna awezae kumwongoza. Ninashuhudia ya kwamba hapana mola wa haki isipokuwa Allaah na ninashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake. Allaah amswalie yeye, kizazi chake, Maswahabah zake na kila mwenye kuwafuata kwa wema mpaka siku ya Qiyaamah.

Amma ba´d:

Allaah (Ta´ala) amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na uongofu na dini ya haki ili kuwaondosha watu kutoka gizani na kuwaongoza katika nuru, kwa idhini ya Mola wao, kwenda katika njia [inayoelekeza kwa], Mwenye nguvu na msifiwa. Allaah amemtuma ili aweze kuabudiwa Yeye mwenyewe kwa kukamilisha udhalilikaji na unyenyekevu Kwake Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala) kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake na kutanguliza hayo mbele ya matamanio na shahawa za nafsi. Allaah amemtuma vilevile ili kutimiza tabia njema na kulingania kwayo kwa kutumia kila njia na kubomoa tabia zote mbaya na kutahadharisha nazo kwa kutumia kila njia. Kwa ajili hiyo ndio maana Shari´ah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imekamilika kwa njia zote. Haihitajii kiumbe mwenye kuikamilisha na kuipanga. Ni yenye kutoka kwa mwingi wa hekima na Mjuzi wa yale yote ambayo ni mema kwa waja Wake na ni Mwenye kuwahurumia.

Mfano mmoja wa tabia hizo nzuri alizotumwa nazo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni haya ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameifanya kuwa ni sehemu katika imani. Hakuna yeyote mwenye kupinga ya kwamba Shari´ah na desturi vyote viwili vimemwamrisha mwanamke kuwa na haya na kuwa na tabia nzuri yenye kumkinga na kutumbukia kwenye fitina na hali zenye utata. Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote kwamba katika aina kubwa za kuwa na haya na kujiheshimisha ni pamoja na yeye kujisitiri ikiwa ni pamoja vilevile na kufunika uso wake kwa kuwa limnamlinda na kumkinga na kutumbukia kwenye fitina.

Hapo kabla watu katika mji huu uliobarikiwa – mji wa Wahyiy, ujumbe, haya na heshima – walikuwa ni wazuri katika suala hili. Wanawake walikuwa wakitoka wakiwa na Jilbaab, mbali kabisa na wanaume. Hali bado ni yenye kuendelea hivo katika miji mingi ya kifalme na himdi zote ni Zake Allaah. Lakini pale baadhi ya watu walipozungumzia juu ya Hijaab, kuwatazama wale wasiofanya hivo na kuonelea kuwa ni sawa kwa mwanamke kuonesha uso, ndipo baadhi ya watu wakaanza kutilia shaka Hijaab na kama ni wajibu kufunika uso au imependekezwa. Au ni jambo tu ambalo ni la kimila na kidesturi na sio wajibu wala haikupendekezwa?

Ili kuondoa shaka hii na kubainisha uhakika wa mambo ndipo nikapendelea kuandika yenye kuweka wazi hukumu kwa kutaraji ya kwamba Allaah (Ta´ala) ataifanya iweke haki wazi na kutufanya sisi ni wenye kuongoka na kuiona haki na kuifuata na batili na kuiepuka. Hivyo basi, ninamuomba Allaah mafanikio na kusema:

Enyi waislamu! Tambueni ya kwamba mwanamke kujisitiri na kuufunika uso wake mbele ya wanaume ajinabi ni jambo la wajibu. Uwajibu wake unatolewa dalili na Kitabu cha Mola Wako (Ta´ala), Sunnah za Mtume Wako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtazamo sahihi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hijaab, uk. 3-5
  • Imechapishwa: 30/10/2016