Ajihadhari tahadhari kubwa kabisa dhidi ya kukusudia kwake kujiongezea wanafunzi na wale wanaokuja kumtembelea. Ajihadhari na kuchukia kwake kusoma kwa wanafunzi wake kwa mwingine miongoni mwa wanaonufaika naye. Hili ni msiba ambao baadhi ya walimu wajinga hujaribiwa nao. Nayo ni dalili iliyo wazi kutoka kwa mwenye nayo juu ya ubaya wa nia yake na uharibifu wa ndani yake. Bali ni hoja iliyo wazi kabisa juu ya kutokukusudia kwake kwa kufundisha kwake uso wa Allaah (Ta´ala) Mtukufu, kwa sababu lau angemkusudia Allaah kwa kufundisha kwake basi asingelichukia jambo hilo. Bali aingeisemeza nafsi yake kwamba yeye amekusudia utiifu kwa kule kufundisha kwake, jambo ambalo tayari limepatikana, na yule mwengine amekusudia kwa kusoma kwake kwa mwingine kuongeza elimu. Kwa hiyo hakuna lawama juu yake.

Tumesimuliwa katika ”al-Musnad” ya Imaam Abu Muhammad ad-Daarimiy – ambaye kuna maafikiano juu ya hifdhi na uongozi wake – ya kwamba ´Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Enyi wabebaji wa elimu! Ifanyieni kazi! Kwani mwanachuoni ni yule anayefanyia kazi yale aliyoyajua na elimu yake ikaenda sambamba na matendo yake. Watakuja watu watakaobeba elimu ambayo haitavuka koo zao. Matendo yao yanapingana na elimu yao, undani wao unapingana na uinje wao. Wanakaa katika vikundi wakijifakharisha wao kwa wao, mpaka itafikia kwamba mtu anamghadhibikia jirani yake kwa sababu tu ameenda kukaa kwa mwingine na kumwacha. Hao matendo yao hayapandi katika vikao vyao hivyo kwa Allaah (Ta´ala).”

Imesihi kwamba Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Nilitamani viumbe wajifunze elimu hii kwa sharti kwamba kusiwepo herufi hata moja itayohusishwa kwangu.”[1]

Kwa maana elimu na vitabu vyake.

[1] Hilyat-ul-Awliyaa’ (13342).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 18/08/2026