Hapaswi kukusudia kwa hilo kufikia lengo miongoni mwa malengo ya kilimwengu kama mali, uongozi, heshima, kujikweza juu ya wenzake, kusifiwa kwa watu, kuelekeza nyuso za watu kwake au mfano wa hayo. Msomaji wa Qur-aan asichanganye kisomo chake na tamaa ya kupata manufaa kutoka kwa baadhi ya wanaomsomea, ni mamoja manufaa hayo ni mali au huduma, makubwa au madogo, hata ikiwa ni kwa namna ya zawadi, ambayo lau si kumsomea basi asingempa. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ

 “Yeyote mwenye kutaka mavuno ya Aakhirah basi Tunamzidishia katika mavuno yake na yeyote mwenye kutaka mavuno ya dunia, tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote.”[1]

مَّن كَانَ يُرِيدُ الْعَاجِلَةَ عَجَّلْنَا لَهُ فِيهَا مَا نَشَاء لِمَن نُّرِيدُ

“Yeyote anayetaka [starehe za dunia] ipitayo upesi, basi Tunamharakizia humo tuyatakayo na kwa tumtakaye.”[2]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kujifunza elimu inayotafutwa kwa ajili ya uso wa Allaah (Ta´ala) ambayo hajifunzi nayo isipokuwa ili kupata kwayo sehemu ya dunia, basi hatapata harufu ya Pepo siku ya Qiyaamah.”

Ameipokea Abu Daawuud kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Kuna Hadiyth nyingi mfano wa hizo.

Anas, Hudhayfah na Ka´b bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anhum) wamesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kutafuta elimu ili abishane nayo na wapumbavu, ajilinganishe nayo na wanazuoni au aelekeze nyuso za watu kwake, basi ajiandalie makazi yake Motoni.”[3]

Ameipokea at-Tirmidhiy kupitia kwa Ka´b bin Maalik kwa tamlo lisemalo:

“Yule mwenye kutafuta elimu ili abishane nayo na wapumbavu, ajilinganishe nayo na wanazuoni au aelekeze nyuso za watu kwake, basi amwingize Motoni.”[4]

[1] 42:20

[2] 17:18

[3] Abu Daawuud (3664) na Ibn Maajah (252). Swahiyh kupitia nyenginezo kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (105).

[4] at-Tirmidhiy (2655). Swahiyh kupitia nyenginezo kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (106).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 18/08/2026