Mlango huu pamoja na milango miwili inayofuata, ndio kusudio la kitabu. Nao ni mrefu na wenye kuenea sana. Hivyo ninaashiria makusudio yake kwa mukhtaswari katika vipengele ili iwe rahisi kuhifadhi na kuudhibiti.

Mosi linalompasa mwalimu wa Qur-aan na msomaji ni kulenga kwa hilo radhi za Allaah (Ta´ala). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini kwa kujiengua na shirki na kuelemea Tawhiyd, na wasimamishe swalah na watoe zakaah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.”[1]

Mtume waa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika matendo hutegemea nia na kila mmoja atalipwa kutokana na vile alivyonuia.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Hadiyth hii ni katika misingi ya Uislamu.

Tumesimuliwa kwamba Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu) amesema:

”Hakika mtu hupewa kwa kadiri ya nia yake.”[3]

Wengine wamesema:

”Hakika watu hupewa kwa kadiri ya nia zao.”

Abul-Qaasim al-Qushayriy amesema:

“Utakasifu wa nia ni kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah kwa makusudio. Maana yake ni mtu alenge kwa utiifu wake kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala) pasi na kitu kingine, kama kujionyesha kwa viumbe, kutafuta sifa njema kwa watu, kupendwa au kusifiwa na viumbe au maana yoyote nyingine isipokuwa kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala).”

Amesema tena:

”Inaweza pia kusemwa kwamba utakasifu wa nia ni kusafisha tendo kutokana na uangaliaji wa viumbe.”

Hudhayfah al-Mar‘ashiy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Utakasifu wa nia ni kufanana kwa matendo ya mja katika dhahiri na ndani.”

Dhuun-Nuun (Rahimahu Allaah) amesema:

”Mambo matatu ni katika alama za utakasifu wa nia: kufanana sifa na kusemwa vibaya kutoka kwa watu wa kawaida, kusahau kuzingatia matendo katika matendo na kutegemea malipo ya matendo Aakhirah.”

al-Fudhwayl bin ‘Iyaadhw (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuacha kitendo kwa ajili ya watu ni kujionyesha. Kufanya kitendo kwa ajili ya watu ni shirki. Utakasifu wa nia ni Allaah kukuokoa na hayo yote mawili.”

Sahl at-Tustariy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Wenye akili walitazama katika tafsiri ya utakasifu wa nia na hawakupata isipokuwa maana nyingine isipokuwa kwamba iwe harakati na utulivu wake wa ndani na wa nje iwe ni kwa ajili ya Allaah (Ta´ala) pekee, bila kuchanganyika na nafsi, matamanio wala dunia yoyote.”

as-Sarriy (Rahimahu Allaah)) amesema:

”Usifanye chochote kwa ajili ya watu, usiache chochote kwa ajili yao, usitoe chochote kwa ajili yao na wala usifunue chochote kwa ajili yao.”

al-Qushayriy amesema:

”Aina bora ya kweli ni kufanana kwa siri na wazi.”

al-Haarith al-Muhaasibiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mkweli ni yule ambaye hajali hata akipoteza hadhi yake yote katika nyoyo za viumbe kwa ajili ya kusahihisha moyo wake. Hapendi watu wajue hata chembe ndogo ya matendo yake mazuri. Wala hachukii watu kujua mabaya yake, kwa sababu kuchukia kwake hilo ni dalili kwamba  anatamani kupaka upendeleo zaidi kwao.  Hili si katika tabia za wakweli.”

Wengine wamesema:

”Ukimtafuta Allaah (Ta´ala) kwa ukweli, basi atakupa kioo utakachoona ndani yake kila kitu cha ajabu katika ulimwengu na Aakhirah.”

Maneno ya Salaf katika hili ni mengi. Tumetaja tu baadhi yake kwa ishara ili kufahamisha lengo. Nimetaja sehemu ya hayo pamoja na maelezo yake mwanzoni mwa maelezo ya ”al-Muhadhdhab” ambamo nikaunganisha humo adabu za mwalimu, mwanafunzi na mwanachuoni, mambo ambayo hatakiwi kuyakosa mwanafunzi – na Allaah ndiye Mjuzi zaidi.

[1] 98:5

[2] al-Bukhaariy (1) na Muslim (1906).

[3] ad-Daarimiy (375).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 18/08/2026