09. Ni ipi hukumu ya kuvuta sigara na kuiuza?

Swali 09: Ni ipi hukumu ya kuvuta sigara na kuiuza?

Jibu: Kuuza sigara ni haramu na vivyo hivyo inahusu kuinunua, kuiuza, kuwakodishia maduka wale wauzaji kwa sababu kufanya hivo maana yake ni kusaidiana katika dhambi na uadui. Dalili ya uharamu wake ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا تُؤْتُوا السُّفَهَاءَ أَمْوَالَكُمُ الَّتِي جَعَلَ اللَّـهُ لَكُمْ قِيَامًا

“Wala msiwape wasiokomaa kiakili mali yenu ambayo Allaah ameifanya kuwa ni kisaidizi chenu cha maisha.”[1]

Dalili tumetumia ni kwa njia ya kwamba Allaah (Ta´ala) ametukataza kuwapa wapumbavu mali, kwa sababu mpumbavu atazitumia katika mambo yasiyokuwa na manufaa. Aidha amebainisha (Subhaanah) ya kuwa fedha hizi watu wanazitumia katika mambo yenye manufaa katika dini na dunia yao. Kwa maana nyingine kuzitumia katika sigara hakuna manufaa katika dini wala dunia. Kwa hivyo kuzitumia katika jambo hilo kunapingana na yale aliyowawekea Allaah (Ta´ala) Shari´ah waja Wake. Miongoni mwa dalili za uharamu wake ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ

“Wala msiziue nafsi zenu.”[2]

Kinacholengwa katika Aayah ni kuwa ni jambo limethibiti kidaktari ya kwamba uvutaji sigara unapelekea katika maradhi yasiyopona yanayompelekea mwenye nayo kwenye kifo kama vile kansa. Kwa hiyo mwenye kuitumia amefanya sababu ya kumwangamiza. Dalili nyingine ya uharamu wake ni maneno Yake (Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ

“Kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu. Kwani Yeye hapendi wanaofanya israfu.”[3]

Kinacholengwa katika Aayah hii ni kwamba ikiwa Allaah amekataza israfu katika mambo yanayofaa, basi makatazo ya kutumia pesa katika mambo yasiyokuwa na manufaa yatakuwa na nguvu zaidi.

Miongoni mwa dalili za uharamu wake ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuharibu pesa. Hapana shaka yoyote kwamba kutumia mali katika kununua sigara ni kuharibu pesa. Pesa ikitumiwa katika mambo yasiyokuwa na faida yoyote basi huko ni kuiharibu kusikokuwa na shaka. Zipo dalili nyinginezo. Akili inatosheka na dalili moja kutoka katika Kitabu cha Allaah au kutoka katika Sunnah zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuhusu mtazamo sahihi unaofahamisha juu ya uharamu wake ni kwamba kila mwenye busara hawezi kutumia kitu ambacho kinampelekea kuumwa na kuuguwa. Kwa sababu ni lazima kwa mwenye akili kuhifadhi mwili na pesa zake. Hakuna anayepuuza hilo isipokuwa ambaye ni punguani katika akili na kufikiria kwake.

Dalili za kinadharia juu ya uharamu wake ni kwamba mvutaji akikosa sigara basi anahisi dhiki moyoni mwake, mkanganyiko na mawazo na moyo wake hauchamgamki isipokuwa akiipata. Miongoni mwa dalili za kinadharia juu ya uharamu wake ni kwamba mvutaji hupata ugumu wa kufanya ´ibaadah na khaswa swawm. Mvutaji hupata uzito mkubwa wa kufunga kwa sababu amezuiwa kuivuta kuanzia kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua. Katika kipindi cha majira ya joto ambapo mchana unakuwa mrefu pengine swawm inakuwa yenye kuchukiza kwake.

Mimi nawanasihi ndugu zangu waislamu wote kwa jumla na khaswa wale waliopewa mtihani watahadhari kutokana na jambo hilo. Ni mamoja kwa njia ya kununua, kuuza, uvutaji na kukodisha maduka kwa ajili ya kufanya biasara hiyo na kusaidia kwa njia yoyote ile.

[1] 04:05

[2] 04:29

[3] 07:31

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 01/03/2023