… kufufuliwa baada ya mauti… – Ahl-us-Sunnah wanaamini msingi wa tano ambao ni kuamini siku ya Mwisho au kufufuliwa baada ya kufa. Ahl-us-Sunnah wanaamini kuwa majini na watu watakufa na kwamba watafufuliwa.

Mtu anaweza kusema ´kufufuliwa Aakhirah` na pia mtu anaweza kusema ´siku ya Mwisho`. Yote mawili yamekuja katika maandiko. ´Siku ya mwisho` ni jina limekuja kwa dalili ya Qur-aan na katika baadhi ya Hadiyth kumekuja jina ´kufufuliwa baada kufa`.

Ahl-us-Sunnah wanaamini kuwa wanaadamu na majini watakufa kisha baada ya hapo watafufuliwa. Halafu waende kulipwa kwa ajili ya matendo yao ya kheri na ya shari. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amebainisha hilo pale aliposema:

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu, bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda – na hayo kwa Allaah ni mepesi.” (64:07)

Ni lazima watu wafufuliwe na kulipwa.

Kwa hivyo siku ya Mwisho ni kule kufufuliwa baada ya kufa. Hapo ndipo watu watalipwa kwa matendo yao, ambaye alitenda mema atalipwa mema na ambaye alitenda maovu atalipwa maovu. Amesema (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

“Na ni vya Allaah Pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili Awalipe [adhabu ya Moto] wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda na ili Awalipe wale waliofanya wema kwa [kuwaingiza] Peponi.” (53:31)

Muumbaji ana miadi ambayo ni siku ya Qiyaamah hata kama duniani anaweza kuwaacha. Ikiwa kuna watu watakufa pasi na kuadhibiwa, basi wana miadi. Amesema (Subhaanah):

وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّـهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ

“Na wala usidhanie kwamba Allaah Ameghafilika na yale wanayoyatenda madhalimu. Hakika Anawaakhirisha kwa ajili ya Siku ambayo macho yatadokoka [kwa kiwewe kubwa].” (14:42)

Bi maana siku ya Qiyaamah.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com