Tawhiyd hii, kwa aina zake zote na haki zake zote, ndani yake inalengesha neno moja: hapana mungu isipokuwa Allaah. Ndani yake mna kukanusha نفيا na kuthibitisha إثباتا. Bi maana linakanusha waungu wengine wote wasiokuwa Allaah na badala yake linamthibitishia Allaah mmoja pekee. Vilevile ndani yake kuna kupenda na kuchukia. Kumpenda Allaah na kumchukia mwingine asiyekuwa Allaah.

Dini ya Tawhiyd imejengwa juu ya misingi hii miwili. Hivyo ndivyo amesema (Ta´ala) kuhusu kipenzi Chake Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba aliwaambia watu wake:

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَ إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ

“Ibraahiym alipomwambia baba yake na watu wake: “Hakika mimi ni mwenye kujiweka mbali kabisa na yale mnayoyaabud. Isipokuwa Ambaye ameniumba, basi hakika Yeye ataniongoza.”[1]

Huu ndio mwenendo wa kila Mtume ambaye alitumilizwa na Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.”[2]

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا

“Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah, kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika.”[3]

Kwa hiyo mwenye kusema “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” basi ametangaza kujitenga mbali na kila ambaye si Allaah na atalazimika kumtekelezea ´ibaadah Allaah. Hiyo ni ahadi anayofunga mtu na nafsi yake mwenyewe:

فَمَن نَّكَثَ فَإِنَّمَا يَنكُثُ عَلَىٰ نَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللَّـهَ فَسَيُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا

“Basi atakayevunja ahadi, hakika si vinginevyo isipokuwa anavunja dhidi ya nafsi yake na yeyote atimizaye yale aliyomuahidi Allaah, basi Atampa ujira mkubwa.”[4]

Kutamka “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” ni kutanganza Tawhiyd-ul-´Ibaadah. Kwa sababu mungu maana yake ni mwabudiwa. Kwa msemo mwingine maana yake ni “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah”.

[1] 43:26-27

[2] 16:36

[3] 02:256

[4] 48:10

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 14
  • Imechapishwa: 25/03/2019