09. Barua ya wazi ya Ibn Laadin kwa imaam Ibn Baaz

Ndugu yangu Muislamu! Tazama sasa ni nini Usaamah bin Laadin alichomwandikia Imaam na Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz (Rahimahu Allaah) ambaye anaheshimiwa na ulimwengu mzima wenye kukubali elimu yake iliyobobea, ustahiki wake juu ya fatwa na kuwatakia kwake wema watu wote. Aliandika kwenye ilani (12) pindi alipokuwa akimpa mawaidha na kumfanya kuwa ni mjinga:

“Sisi – kamati ya an-Naswiyhah wal-Iswlaah – hapo kabla tuliwaandikia barua ya wazi katika ilani yetu (11) na kuwakumbusha kwa jina la Allaah juu ya wajibu wenu wa Kishar´ah kuhusiana na dini na Ummah. Humo tuliwazindueni juu ya fataawa zenu nyingi na msimamo wenu ambao umepelekea katika madhara ya khatari na yaliyo makubwa katika Ummah wa Kiislamu na wanachuoni na walinganizi wenye kutumikia hilo…

Kwa ajili hiyo sisi tunauzindua Ummah juu ya khatari inayopatikana katika fataawa hizi batili zisizotimiza masharti. Badala yake tunauita Ummah kurejea katika wale ambao wana elimu ya Kishari´ah na umaizi wa mambo ya kisasa wakati wanapotaka fatwa.

Hali kadhalika tunazidi kukariri wito wetu kwako, ee Shaykh, kutoka kwenye mashimo ya watawala hawa. Wamekupanga ili utumikie matamanio yao. Wanakutumia dhidi ya kila mlinganizi na mtengenezaji. Tunakukumbusha hali za wale ambao Allaah amesema juu yake:

لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۙ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ

“Ili wabebe mizigo [ya madhambi] yao kamili Siku ya Qiyaamah, na mizigo ya wale waliowapoteza bila ya elimu. Tanabahi! Uovu ulioje wanayoyabeba.” (16:25)

Ee Shaykh! Kwa kumalizia barua hii ninasema kukwambia: Ikiwa hamuwezi kusimamia haki wazi wazi na kuwanusuru watu wake dhidi ya watawala basi angalau mnaweza kuacha nafasi hizo rasmi ambazo mamlaka wamewachafulia nazo. Jiwekeni mbali na milango ya viongozi hawa ambao wamempiga vita Allaah wazi wazi ili msifikwe na yatayowafika. Shikamaneni na njia ya uongofu iliyotaja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa juu yake:

“Uchunge ulimi wako, baki nyumbani kwako na lia juu ya madhambi yako.”[1]

Imepokelewa na at-Tirmidhiy na ipo katika “Swahiyh-ul-Jaami´ as-Swaghiyr”.

Tarehe 1415-05-28/1995-01-29

Usaamah bin Muhammad bin Laadin”

Tunajikinga kwa Allaah kutokana na maradhi ya kiburi ambayo yanafanya kutupilia mbali haki na kuwadharau watu. Yanasababishwa na vifundo, kuwaona chini watu na chuki juu ya watu wenye fadhila na wenye kuamini na kumcha Allaah.

[1] Ahmad (17488).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Waqafaat wa Ma´aalim, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 13/01/2015