08. Uwajibu wa kuthibitisha majina na sifa za Allaah

Miongoni mwa mambo inapelekea shahaadah ni kuthibitisha majina na sifa za Allaah ambazo amejiita na kujisifu nazo Mwenyewe au amemwita na kumsifu nazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَاۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”Hakika Allaah ana majina mazuri mno kabisa, hivyo basi muombeni kwayo. Waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.” (07:180)

Amesema [´Abdur-Rahmaan bin Hasan] katika “Fath-ul-Majiyd”:

“Msingi wa kupotosha (الْإِلْحَاد) katika maneno ya waarabu ni kwenda kinyume na malengo, kupinda, jeuri na kupinda. Majina na sifa za Mola (Ta´ala) zote ni majina na sifa alizowajuza waja Wake na zote zinafahamisha juu ya ukamilifu Wake (Jalla wa ´Alaa).”[1]

Amesema tena (Rahimahu Allaah):

“Kupotosha ndani yake kuna kuyakanusha na kuyapinga, kuharibu na kukanusha maana yake, kuyapotosha kutokamana na usawa na kuyatoa katika haki kwa kuyapindisha maana au kuyafanya ni majina ya viumbe hawa kama uharibifu wa Ahl-ul-Ittihaad ambao wameyafanya kuwa ni majina ya viumbe hawa wazuri wao au wabaya wao.”[2]

Kwa hivyo yule mwenye kupotosha majina na sifa za Allaah kwa kukanusha, kupindisha maana au kumtegemezea maana yake Allaah na wakati huohuo asiamini ile maana yake tukufu inayofahamishwa nayo – katika Jahmiyyah, Mu´tazilah na Ashaa´irah – basi amekwenda kinyume na yale yanayofahamishwa na shahaadah. Kwa sababu mungu ni yule anayeombwa na kunafanywa Tawassul kupitia majina na sifa Zake. Amesema (Ta´ala):

فَادْعُوهُ بِهَا

”Hivyo basi muombeni kwayo.”

Asiyekuwa na majina na sifa ni vipi atakuwa mungu? Vipi ataombwa? Ataombwa kwa kitu gani? Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Watu wamevutana katika hukumu nyingi na hawakuvutana sehemu hata moja katika Aayah zinazozungumzia sifa za Allaah na maelezo yake. Bali Maswahabah na wanafunzi wao wameafikiana juu ya kuyakubali na kuyapitisha pamoja na kuelewa maana yake na kuthibitisha uhakika wake. Hii ni dalili inayofahamisha kuwa ni aina mbili kubwa zaidi [ya Aayah] zilizokuwa wazi na kutilia umuhimu ubainifu wake ni jambo muhimu zaidi. Kwa kuwa ni katika ukamilifu wa kuhakikisha shahaadah na kuyathibitisha ni katika mambo yanayopelekea Tawhiyd. Hivyo Allaah (Subhaanah) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakabainisha ubainifu wenye kutosheleza usiokuwa ndani yake na utatizi.

Kuna uwezekano kukawepo baadhi ya  Aayah za hukumu ambazo hazifahamiki na baadhi ya watu. Kuhusu Aayah zinazozungumzia sifa za Allaah wasomi na wasiokuwa wasomi wote wanashirikiana katika kufahamu maana yake. Namaanisha kufahamu maana yake na si kufahamu namna yake.”[3]

Amesema vilevile:

“Hili ni jambo linalojulikana kwa maumbile, akili timamu na Vitabu vya mbinguni ya kwamba yule mwenye kukosa sifa kamilifu hawi mungu, mwendeshaji wala mola. Bali ni mwenye kusemwa vibaya, aliye na kasoro na mapungufu. Hastahiki kuhimidiwa duniani wala Aakhirah. Anayestahiki kuhimidiwa duniani na Aakhirah ni yule aliye na sifa kamilifu na tukufu ambazo kwazo ndio akawa ni mwenye kustahiki kuhimidiwa. Kwa ajili hii ndio maana Salaf wameita vitabu vyao walivyotunga katika ´Aqiydah na kuthibitisha sifa za Mola, kuwa Kwake juu ya viumbe Wake, maneno Yake na maneno Yake “Tawhiyd”. Kwa kuwa kuyapinga, kuyakanusha na kuyakufuru hayo ni kumkanusha na kumkana Muumbaji. Mambo yalivyo ni kwamba Tawhiyd ni kule kuthibitisha sifa za ukamilifu Wake na kumtakasa kutokamana na ushabihiano na mapungufu.”[4]

[1] Fath-ul-Majiyd (02/742-743).

[2] Badaa´i-ul-Fawaa-id (01/169).

[3] Mukhtaswar Swawaa´iq-ul-Mursalah (01/15).

[4] Madaarij-us-Saalikiyn (01/26).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ma´naa laa ilaaha illa Allaah, uk. 28-31
  • Imechapishwa: 23/09/2023