Msafiri ni kama tulivyosema kwamba imeruhusiwa kwake kula. Ili msafiri apate ruhusa ya kuweza kuacha kufunga inatakiwa iwe ni ile safiri inayomruhusu kufupisha na kukusanya swalah. Ni jambo ambalo wanachuoni wametofautiana juu yake. Baadhi wanaonelea kuwa itakuwa inaruhusiwa ikiwa safari umbali wake ni wa siku mbili kwa kutembea na miguu. Wengine wanamaanisha kwamba ni pale ambapo safari umbali wake utakuwa wa mchana na usiku mmoja. Haya yametajwa katika upokezi kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho kusafiri umbali wa siku tatu isipokuwa awe pamoja naye Mahram.”[1]

Kumekuja upokezi vilevile unaotaja “mchana na usiku mmoja”[2], “siku moja”[3] na “usiku mmoja”[4]. Mapokezi yote haya yametajwa na al-Bukhaariy na Muslim. Kuna upokezi uliyoko kwa Abu Daawuud unaotaja umbali sawa na takriban kilomita 20. Katika mtiririko wa wapokezi yupo mtu anayeitwa Suhayl bin Abiy Swaalih ambaye amepwekeka katika kuipokea na hali yake imetiwa dosari.

Kwa kufupisha ni kwamba tunatakiwa kuchukua ule umbali mdogo unaoitwa “safari”. Safari kama hiyo ni mchana mtimilifu au usiku mtimilifu, ambao ni sawa na kilomita 40. Kwa msemo mwingine ni kwamba mtu ambaye anasafiri kilomita 40 anaruhusiwa kuacha kufunga na kufupisha swalah.

Pengine mtu akasema kuwa safari za leo zinatofautiana na safiri za wakati wa kale. Ni kweli na hii ni neema ya Allaah (´Azza wa Jall). Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa juu ya kufupisha swalah wakati wa khofu baada ya khofu kwisha, akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ni swadaqah ambayo Allaah amekupeni. Kwa hivyo ikubalini swadaqah Yake.”[5]

[1] Ahmad (8564).

[2] al-Bukhaariy (1088) na Muslim (1339).

[3] Muslim (1339).

[4] Muslim (1339).

[5] Muslim (686).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tafsiyr Aayaat-is-Swiyaam, uk. 14-16
  • Imechapishwa: 02/06/2017