08- Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisimama karibu na Sutrah. Baina yake yeye na ukuta ilikuwa dhiraa tatu[1].

Baina ya sehemu alipokuwa akisujudu na ukuta alikuwa akiweza kupita kondoo[2].

Vilevile alikuwa akisema:

“Usiswali bila ya Sutrah na usimwache yeyote akupite mbele. Akikataa, pambana naye, kwani yuko pamoja na rafiki.”[3]

Mmoja wenu akiswali kwenye Sutrah, basi aijongelee. Shaytwaan hatoikata swalah yake[4].

Wakati mwingine alikuwa akiswali karibu na nguzo iliyo msikitini kwake[5].

Alipokuwa akiswali [kwenye sehemu ya wazi ambako hakuna Sutrah mbele yake] alikuwa akiuchomoke mkuki mbele ardhini na akiswali kuuelekea na watu wanaswali nyuma yake, na watu wakipita nyuma yake[6].

Wakati mwingine alikuwa akimtenga mnyama wake na akiswali kuuelekea[7].

Hata hivyo hili ni tofauti na kuswali kwenye vibanda vya ngamia, kwani hilo amelikataza[8].

Wakati mwingine alikuwa akichukua tandiko la ngamia, akaliweka wima na kuswali kuelekea ncha yake[9].

Alikuwa akisema:

“Mmoja wenu atapoweka kitu mbele yake kama kiti cha nyuma cha tandiko la ngamia, aswali na wala asijali atayepita nyuma yake[10].

Siku moja aliswali kuuelekea mti[11].

Mara nyingine alikuwa akiswali kuelekea kitanda na ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amelala juu yake [akiwa amejifunika shuka][12].

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haachi kitu kipite baina yake na Sutrah[13].

Siku moja alipokuwa anaswali akaja kondoo anakimbia anataka kupita mbele yake. Upesi akamuwahi mpaka akalibonyeza tumbo lake ukutani [na akawa amepita nyuma yake].

Siku moja aliswali swalah ya faradhi na akakunja ngumi. Baada ya swalah, wakasema: “Ee Mtume wa Allaah, kumetokea kitu katika swalah?” Akasema: “Hapana. Ni shaytwaan tu aliyekuwa anataka kupita mbele yangu. Nikamkaba shingoni mpaka nikahisi ubaridi wa ulimi wake mkononi mwangu. Ninaapa kwa Allaah! Kama isingekuwa ndugu yangu Sulaymaan kunitangulia basi ningemfunga kwenye nguzo ya msikiti mpaka watoto wa al-Madiynah wakazunguka naye. [Anayeweza kuzuia kusipite chochote baina yake yeye na Qiblah na afanye hivo.”[14]

Alikuwa akisema:

“Mmoja wenu ataposwali kuelekea Sutrah inayomsitiri yeye kutokamana na watu na akataka mtu kupita mbele yake, basi amsukume kifuani mwake na [na amzuie kadiri na awezavyo] (na katika upokezi mwingine “amzuie” mara mbili). Atapokataa, basi apambane naye kwani hakika yeye si vyengine ni shaytwaan.”[15]

Alikuwa akisema:

“Lau yule mwenye kupita mbele ya mwenye kuswali angejua dhambi anazopata, kusimama arubaini ingelikuwa ni bora kwake kuliko kupita mbele yake.”[16]

[1] al-Bukhaariy na Ahmad.

[2] al-Bukhaariy na Muslim.

[3] Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” yake (1/93/1) kwa isnadi nzuri.

[4] Abuu Daawuud, al-Bazzaar (uk. 54) na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy na an-Nawawiy wameafikiana naye.

[5] Ibn Haani’amesema katika ”al-Masaa’il ´an al-Imaam Ahmad” yake [(1/66) chapa ya al-Maktab al-Islaamiy]:

“Siku moja nilikuwa pamoja na Abu ´Abdillaah (anamaanisha Imaam Ahmad) kwenye msikiti mkuu na akaniona naswali bila ya Sutrah mbele yangu. Akanambia: “Weka Sutrah mbele yako.”Nikamfanya mtu kama Sutrah.”

[6] al-Bukhaariy, Muslim na Ibn Maajah.

[7] al-Bukhaariy na Ahmad.

[8] al-Bukhaariy na Ahmad.

[9] Muslim, Ibn Khuzaymah (2/92) na Ahmad.

[10] Muslim na Abuu Daawuud.

[11] an-Nasaa’iy na Ahmad kwa isnadi Swahiyh.

[12] al-Bukhaariy, Muslim na Abuu Ya´laa (3/1107).

[13] Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” yake (1/95/1), at-Twabaraaniy (3/140/3) na al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

[14] Ahmad, ad-Daaraqutwniy na at-Twabaraaniy kwa isnadi Swahiyh.

Maana ya Hadiyth hii imetajwa vilevile katika al-Bukhaariy na Muslim kupitia kundi la Maswahabah na ni moja katika Hadiyth nyingi ambazo Qaadiyaaniyyah hawaiamini. Hawaamini ulimwengu wa majini uliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah. Mfumo wao wa kuyapinga maandiko [ya Qur-aan na Sunnah] ni wenye kujulikana. Wamepotosha Aayah:

قُلْ أُوحِيَ إِلَيَّ أَنَّهُ اسْتَمَعَ نَفَرٌ مِّنَ الْجِنِّ

“Sema: “Nimefunuliwa Wahy juu ya kundi miongoni mwa majini… “” 72:01

na kusema kwamba maana yake ni wanaadamu. Wamefanya neno “majini” kuwa ni visawa vya “wanaadamu” na hivyo wakawa wameiacha njia ya lugha na Shari´ah. Hali kadhalika inahusiana na Sunnah. Wakiweza kuyapotosha kwa tafsiri batili, basi wanafanya hivo. Vinginevyo ni rahisi sana kwao kuvihukumu kuwa ni batili hata kama watakusanyika maimamu wa Hadiyth na Ummah mzima nyuma yao na kusema ni Swahiyh na yamepokelewa kwa mapokezi mengi. Allaah awaongoze!

[15] al-Bukhaariy na Muslim.

[16] Ibn Khuzaymah (1/94/1).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 82-84
  • Imechapishwa: 13/10/2016