08. Sababu ya nne ya talaka ambayo ni tahamaki mke kumchukia mume

4 – Kuchukiana na kutoendana

Jambo hilo linampelekea mke kutosimamia wajibu wa mume. Mwanaume na mwanamke wameoana bila kulazimishwa na wameoana kwa kupendana. Wanaeshi pamoja miaka na miezi kadhaa, hata hivyo ikatokea mwanamke akamchukia na akakhofia asitimize haki yake inayompasa. Matokeo yake akalazimika kuomba talaka na kwa kutumia nguvu. Katika hali kama hii inafaa kwake mwanamke kuomba talaka akichelea juu ya nafsi yake kutomtekelezea haki inayompasa. Kama ilivyokuja katika kisa cha mwanamke wa Thaabit bin Shammaas (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia:

”Nilimwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Naapa kwa Allaah, simtii dosari katika tabia wala dini. Nachelea kufuru katika Uislamu.”[1]

Bi maana aliona kile kitendo cha yeye kumuasi mume wake, kutompa haki yake na kutotekeleza haki yake kuwa ni kufuru kwa maana ya kwamba hayo ni maasi na dhambi. Ameona kuwa kufanya hivo sio katika dini na akachelea dhambi juu ya nafsi yake. Hivyo akaomba talaka. Itakuja maana ya Hadiyth hii itapofika wakati wake.

Tulicholenga hapa ni kwamba alimchukia. Alikhofia kitu gani? Kutotekeleza wajibu wake na hivyo ndipo akaomba talaka. Hakuna tena mapenzi na mahaba. Kuendelea kuishi tena katika hali kama hii ni kuendelea kuishi ndani ya moto, kwa sababu hamtekelezei haki yake na yeye mume anamwomba haki yake. Hivyo kukawa kuna migongano miwili.

[1] al-Bukhaariy (5673).

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Twalaaq – asbaabuhu wa ´ilaajuh, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 01/04/2024