38 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Mja hatoacha kujibiwa du´aa muda wa kuwa hajaomba jambo lenye dhambi, kukata udugu midhali hatokuwa na haraka.” Wakasema: “Ni vipi atakuwa na haraka, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Husema “Nimeomba, nimeomba na sikuona naitikiwa”. Hapo ndipo akahuzunika na kuacha kuomba.”[1]

Kuna maafikiano juu yake na tamko ni la Muslim.

MAELEZO

Hadiyth inabainisha vikwazo viwili vya kuitikiwa du´aa:

1 – Kuomba jambo lenye dhambi. Kwa mfano mtu akaomba du´aa ya kunywa pombe, kuvuta sigara au kufanya machafu.

2 – Akaomba du´aa ya kukata udugu, jambo ambalo ni dhambi pia ingawa limefanywa kuwa maalum kutokana na umuhimu wake. Kwa mfano mtu akamuombea du´aa ndugu yake asisamehewe na mfano wa hayo.

Vivyo hivo kuchupa mipaka katika du´aa. Kwa mfano mtu akamuomba kupandishwa ngazi za Mitume. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

“Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye hawapendi wenye kuvuka mipaka.”[2]

Mwombaji hatakiwi kufanya haraka na kusema ´nimeomba, nimeomba` na sijaitikiwa. Hapo ndipo akahuzunika na kuacha kuendelea kuomba du´aa. Kinachotakiwa kwa mtu aendelee kuomba du´aa na amsisitize Allaah katika kuomba kwake. Allaah anawapenda wenye kufanya masisitizo katika du´aa zao na wenye kuomba kwa wingi.

Du´aa ina manufaa mengi na faida nyingi hata kama mtu hatoitikiwa. Kuomba du´aa ni ´ibaadah ambayo mja analipwa thawabu juu yake. Wakati mwingine Allaah (´Azza wa Jall) hukucheleweshea kukujibu na hilo likawa ni sababu ya kulainishwa moyo wako na kusamehewa madhambi, au Allaah akakuondoshea mabaya ambayo ni makubwa zaidi kuliko kile ulichokiomba, au akakuhifadhia kheri huko Aakhirah ambayo ni kubwa zaidi.

[1] al-Bukhaariy (6340) na Muslim (2735).

[2] 07:55

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 12/10/2025