08. Kuyakosoa makundi ya Kiislamu ni kusengenya?

Swali 08: Kuna walinganizi ambao wamekosoa kundi linalolingania katika dini ya Allaah. Je, kufanya hivi ni usengenyaji au hapana?

Jibu: Kulingania katika dini ya Allaah ni jambo linatakiwa kuwa katika mipaka Allaah aliyowawekea Mitume wake. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na miungu ya uongo.”[1]

Vilevile Alimuwekea mpaka Mtume wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ndiye Mtume wa mwisho. Amesema (Ta´ala):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖوَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah juu ya ujuzi mimi na anayenifuata. Utakasifu ni wa Allaah nami si miongoni mwa washirikina.””[2]

Kwa hivyo mwenye kuleta mfumo na njia inayoenda kinyume na ya Mitume (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam) basi ni wajibu kwa wanachuoni kubainisha uendaji kinyume na makosa haya. Asiyebainisha ilihali ni mwenye kujua hilo basi anakuwa ni mwenye kupata dhambi. Isipokuwa tu pale ambapo kutakuwepo ubainifu wenye kutosheleza juu ya kundi fulani, katika hali hii itakuwa ni faradhi kwa baadhi ya watu. Kwa maana ya kwamba baadhi wakisimama na kazi hii basi si wajibu kwa wengine. Ama ikiwa waliosimama na kazi hiyo wanahitajia msaada na sapoti, basi ni wajibu kwa watu wote kuwasaidia na kuwasapoti.

Mwenye kudai kuwa haijuzu kuwazungumzia watu hawa ambao wamejiwekea mfumo na njia yenye kwenda kinyume na mfumo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni mwenye kukosea. Anachokusudia ni kuwa anataka kuangusha kazi ya kuamrisha mema na kukataza maovu, kubainisha haki na kusaidiana katika wema na uchaji Allaah. Endapo atakuwa sio mwenye kukusudia hilo basi atakuwa amewaiga wale waliokusudia kufanya hivo na atakuwa amedanganywa. Ni wajibu kwake kurejea katika haki na aachane na msimamo wake wa kuwa haifai kuwakataza wenye kukosea katika mfumo au njia iliyowekwa katika Shari´ah wakati wa kulingania katika dini ya Allaah.

[1] 16:36

[2] 12:108

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fataawaa al-Jaliyyah
  • Imechapishwa: 16/07/2017