07. Imethibiti katika Shari´ah kuwakataza viongozi hadharani?

Swali 07: Ni jambo limethibiti katika Qur-aan na Sunnah kuwakemea watawala hadharani juu ya minbari?

Jibu: Uhakika wa mambo ni kuwa kuwakemea watawala hadharani ni jambo lililozuliwa. Sio katika misingi ya Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tanabahini! Yule ambaye atakuwa na mtawala juu yake na akaona anafanya kitu cha kumuasi Allaah, basi achukie kile anachokifanya na asiondoshe mkono kutoka katika utiifu.”[1]

Hivi ndivyo anavyosema Mtume wa uongofu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hivyo haijuzu kukataza hadharani juu ya minbari. Kuna madhara mengi yanayopelekea katika hilo kuliko faida. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kutoa nasaha kwa watu wote kwa jumla na kwa wale viongozi wao. Tamiym ad-Daariy ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Dini ni kupeana nasaha. Dini ni kupeana nasaha. Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: “Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na watu wa kawaida.”

Lakini hata hivyo haifai kuwapa nasaha viongozi kwa sura na namna yoyote ile. Bali inatakiwa kuwapana nasaha kwa siri ili yule mtawala aweze kuikubali. Hii ndio asli. Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ´anh) alisema pindi alipoambiwa ni kwa nini hamnasihi ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mnadhania kuwa simnasihi mpaka niwasikilizishe?”

Anachotaka kusema ni kuwa anamnasihi kwa siri. Kwa hivyo hii ndio asli katika Sunnah. Ambaye anasimama juu ya minbari na kusema:

“Huu ni ujumbe kwenda kwa mtawala au waziri fulani.”

ni mwenye kukosea. Lililo la wajibu kwake ikiwa anaona kuwa anafanya kitu katika maasi basi amtumie ujumbe kwa siri. Akikubali amshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa hilo na akikataa basi atambue kuwa ametekeleza wajibu wake. Hana juu yake dhambi baada ya kufanya hivi.

[1] Muslim (1855) na Ahmad (23479).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fataawaa al-Jaliyyah
  • Imechapishwa: 16/07/2017