Baada ya an-Nawawiy kutaja hayo maoni ya kwanza na watetezi wake, akasema (Rahimahu Allaah):

”al-Awzaa´iy na Abu Thawr wamesema kwamba mwanzo wa muda ni tangu apanguse baada ya kupatwa na hadathi. Haya ndio maoni yaliyopokelewa kutoka kwa Ahmad na Daawud. Haya ndio yaliyochaguliwa na yene dalili yenye nguvu. Yamechaguliwa na Ibn-ul-Mundhir, ambaye amenukuu mfano wake kutoka kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). al-Maawardiy na ash-Shaashiy wamenukuu kutoka kwa al-Hasan al-Baswriy kwamba mwanzo wake ni tangu kuzivaa.

Wale wenye kusema kwamba muda unaanza tangu upangusaji wa kwanza wamejengea hoja kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msafiri hufuta siku tatu.”

Nazo ni Hadiyth Swahiyh, kama ilivyotangulia.  Hili ni tamko la wazi kwamba anapangusa siku tatu na hili haliwi isipokuwa ikiwa muda utaanza kuhesabiwa tangu upangusaji. Kwa sababu ash-Shaafi´iy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kwamba akipata hadathi katika mji wake na akafuta katika safari, basi anakamilisha kupangusa kama msafiri. Hivyo ameifunganisha hukumu na upangusaji.

Maswahiba wetu wamejengea hoja kwa riwaya aliyoipokea Haafidhw al-Qaasim bin Zakariyyaa al-Mutrazziy kutoka kwa Swafwaan, ambaye amesema:

“Tangu hadathi moja mpaka hadathi nyingine.”

Nayo ni ziada ya ajabu na ambayo haikuthibiti. Aidha wamejengea hoja kwa kipimo.”[1]

[1] al-Majmuu´ (1/470).

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-un-Nush fiy Ahkaam-il-Mash, uk. 89-90
  • Imechapishwa: 27/04/2026