Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

3 – Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Mkiuona fungeni na mkiuona fungueni. Mkifunikwa na mawingu basi ikadirieni.”[1]

 Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Mkifunikwa na mawingu, basi ikadirieni siku thelathini.”[2]

Katika upokezi wa al-Bukhaariy imekuja:

“Mkifunikwa na mawingu, basi kamilisheni idadi ya siku thelathini.”[3]

4 – Amepokea pia kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“… mkamilishe idadi ya Sha´baan siku thelathini.”[4]

Maneno yake ”mkiuona” inamaanisha mwezi mwandamo, kwa kuwa dhamiri inarejea kwenye dhana inayofahamika kutoka muktadha. Ni kama maneno Yake Allaah:

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ

“Hakika Sisi Tumeiteremsha katika usiku wa Qadar.”[5]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea:

“Msifunge mpaka muone mwezi mwandamo.”

Makusudio ni ikiwa mtauona kutoka kwa yule ambaye kunathibiti kuona kwake.

Maneno yake ”Mkifunikwa na mawingu” maana yake ni kwamba mwezi usionekane kutokana na mawingu, vumbi au kitu kingine.

Maneno yake ”basi ikadirieni” maana yake ni kwamba kamilisheni idadi yake ambayo ni siku thelathini kwa mujibu wa mapokezi yaliyotajwa. Maneno hayo yanayo tafsiri nyingine, nayo ni kwamba ibanani. Hilo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ

“… na yule aliyebaniwa riziki yake… ”[6]

Kuibana idadi kunamaanisha kuifanya Sha´baan kuwa siku ishirini na tisa, jambo ambalo litakuja huko mbele.

Hadiyth inafahamisha ulazima wa kufunga Ramadhaan pale kunapothibiti kuonekana mwezi mwandamo na ulazima wa kufungua pale tu utapoonekana mwezi mwandamo wa Shawwaal na kwamba hukumu ya kufunga na kufungua inategemea uonaji hata kwa kutumia vifaa vya macho vinavyokuza vionywa, kwa sababu hilo ni uonaji kwa macho moja kwa moja.

[1] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (1080).

[2] Muslim (1081).

[3] al-Bukhaariy (1907).

[4] al-Bukhaariy (1909) na Muslim (1081).

[5] 97:01

[6] 65:07

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/11-13)
  • Imechapishwa: 30/01/2025