07. Wametoka katika Uislamu kwa sababu ya tafsiri zao

Kuhusu tafsiri ya kundi la tatu na kwamba madhambi yanayokusudiwa ni kwa njia ya kuritadi, ni mbaya zaidi kuliko ya kabla yake. Kwa sababu hiyo ni tafsiri ya Khawaarij. Wametoka nje ya dini kwa sababu ya tafsiri. Matokeo yake wakawakufurisha watu kwa sababu ya madhambi madogomadogo na makubwamakubwa. Unajua yale ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaeleza juu ya utokaji na kuhalalisha kuzimwaga damu zao[1]. Tunajua pia kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amekadhibisha fikira zao na hapo ni pindi alipohukumu mwizi akatwe mkono na mzinzi na anayewarushia wenziwe tuhuma za machafu kuchapwa bakoro. Yangelikuwa madhambi yao yanawafanya wakufuru, basi kusingelikuwa na adhabu nyingine juu yao isipokuwa kuuliwa kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mwenye kubadilisha dini yake muueni.”[2]

Wangelikuwa ni makafiri, basi adhabu yao isingelikuwa kukatwa mkono na kuchapawa bakora. Vilevile Allaah amesema juu ya ambaye amemuua mtu kwa dhuluma:

وَمَن قُتِلَ مَظْلُومًا فَقَدْ جَعَلْنَا لِوَلِيِّهِ سُلْطَانًا

“Na atakayeuliwa kwa kudhulumiwa, basi Tumemfanya msimamizi wake awe na mamlaka.”[3]

Ingelikuwa kuua ni ukafiri, basi ndugu asingelikuwa na haki ya kusamehe wala kuchukua diyaa – badala yake ingelilazimika kumuua aliyeua.

[1] Anaashiria Hadiyth iliyosimulia ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh):

”Watakuja katika zama za mwisho watu ambao meno ndio punde yameota na wenye ndoto za kipumbavu. Watazungumza kwa matamshi ya kiumbe bora kabisa, na wataisoma Qur-aan pasi na kuvuka koo zao. Watatoka katika dini kama ambavo mshale unatoka katika upinde wake. Popote mtapokutana nao, basi waueni. Hakika yule mwenye kuwaua atalipwa thawabu siku ya Qiyaamah.” (al-Bukhaariy (3611) na Muslim (1066))

[2] al-Bukhaariy (3017), Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Ahmad (5/231) kupitia kwa Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) kwa cheni ya wapokezi kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.

[3] 17:33

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 04/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy