07. Ubainifu wa namna Mtume alivokuwa akitawadha

Swali 07: Tunaomba kubainishiwa namna ya kutawadha na kuswali kwa mujibu wa ilivyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokana na haja kubwa ya jambo hilo[1]?

Jibu: Imethibiit kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayojulisha ya kwamba mwanzoni mwa wudhuu´ wake basi anaanza kuosha viganja vyake mara tatu baada ya kunuia wudhuu´ na baada ya kusema “Bismillaah”, kwa sababu ni kitu kilichowekwa katika Shari´ah. Vilevile imepokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia njia nyingi ya kuwa amesema:

“Hana wudhuu´ yule ambaye hakutaja jina la Allaah juu yake.”[2]

Imesuniwa kwa mtawadhaji kutaja jina la Allaah mwanzoni mwa wudhuu´ wake. Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa ni lazima kufanya hivo pale ambapo mtu atakumbuka. Akisahau au akiwa hajui basi hapana neno. Kisha asukutue na apandishe maji puani mara tatu. Kisha aoshe uso wake mara tatu. Kisha aoshe mikono yake kukiwemo viwiko mara tatu. Anatakiwa kuanza mkono wa kuume kisha afuatishe wa kushoto. Kisha afute kichwa chake na masikio yake mara moja. Kisha aoshe miguu yake kukiwemo vifundo vya miguu mara tatu. Ataanza mguu wa kulia. Hapana neno akitosheka mara moja au mara mbili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuna kipindi alitawadha mara mara mojamoja, wakati mwingine mara mbilimbili na wakati mwingine mara tatutatu. Ilikuwa inatokea wakati fulani akitawadha baadhi ya viungo vyake mara mbilimbili na vyengine mara tatutatu. Hayo yanafahamisha kuwa jambo ni lenye wasaa. Lakini kutawadha mara tatutatu ndio bora zaidi. Hapa ni pale ambapo mtu hakwenda haja kubwa wala ndogo. Akifanya moja katika mambo hayo mawili, basi atatakiwa kuanza kutamba kisha atawadhe wudhuu´ uliotajwa.

Kuhusu kutokwa na upepo, kulala, kugusa tupu, kula nyama ya ngamia, yote hayo hayakusuniwa mtu kutamba. Bali itatosha kutawadha wudhuu´ wa kawaida ambao tumetaja. Baada ya kutawadha imesuniwa kwa muumini wa kiume na muumini wa kike kusema:

أشهد أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له وأشهد أن محمدا عبده ورسوله اللهم اجعلني من التوابين واجعلني من المتطهرين

“Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa ni Mmoja hana mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake. Ee Allaah! Nijaalie niwe miongoni mwa wenye kutubu na wenye kujitwahirisha.”[3]

Hayo yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Imewekwa katika Shari´ah kwa mwenye kutawadha kuswali Rak´ah mbili zinazoitwa “Sunnah ya wudhuu´”. Akiswali baada ya kutawadha Sunnah ya Raatibah  basi itamtosheleza na Sunnah ya wudhuu´.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/98-99).

[2] Abu Daawuud (102).

[3] Muslim (234).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 18-20
  • Imechapishwa: 21/02/2022