07. Ni nini maana ya imani kamilifu na inazidi na kupungua?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 7: Ni nini maana ya imani kamilifu na inazidi na kupungua?

Jibu: Imani ni I´tiqaad za moyo na matendo, matendo ya viungo na maneno ya ulimi.

Dini yote, misingi yake na matawi yake vinaingia katika imani.

Ina maana ya kwamba inazidi kwa I´tiqaad yenye nguvu na wingi wake na matendo na maneno mazuri na mengi kama ambavyo inashuka kwa kinyume na hayo.

MAELEZO

Tumeshatangulia kusema kuwa “imani” na “Uislamu” vinaingiliana na kimoja kinaingia ndani ya kingine. Kunapotajwa imani peke yake basi Uislamu unaingia ndani yake. Kunapotajwa Uislamu peke yake basi imani inaingia ndani yake. Isipokuwa tu kunasemwa “imani” na kukakusudiwa yale matendo yaliyojificha, kama hayo yalivotajwa katika Hadiyth ya Jibriyl:

“Imani ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na Qadar; kheri na shari yake.”[1]

Ameeleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba “Uislamu” ni yale matendo yenye kuonekana. Kutamka kwa shahaadah pamoja na imani ya moyo ndio msingi wa “Imani” na “Uisamu”. Kisha kusimamisha swalah, kutoa zakaah na kuhiji. Matendo haya matano yenye kuonekana ndio “Uislamu”.

Imani inazidi na inashuka? Shaykh as-Sa´diy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Imani ni I´tiqaad za moyo na matendo, matendo ya viungo na maneno ya ulimi.

Dini yote, misingi yake na matawi yake vinaingia katika imani.

Ina maana ya kwamba inazidi kwa I´tiqaad yenye nguvu na wingi wake na matendo na maneno mazuri na mengi kama ambavyo inashuka kwa kinyume na hayo.”

I´tiqaad za moyo ndio zile nguzo sita za ”imani” zilizotajwa katika Hadiyth ya Jibriyl. I´tiqaad ya kumwamini Allaah ni kuamini uwepo Wake, kuamini uola Wake, kuamini majina na sifa Zake, kuamini kuwa Yeye pekee ndiye ana haki ya kuabudiwa na kwamba Yeye ndiye Mungu wa haki ambaye ni lazima kuabudiwa kwa kutiiwa, na asiasiwe, atajwe, na asisahauliwe, ashukuriwe na wala asikufuriwe.

Kuwaamini Malaika inapaswa kuamini kwamba wao ni waja watukufu ambao kila mmoja anatekeleza kazi yake aliyopewa na Allaah.

Kuamini Vitabu vilivyoteremshwa kutoka kwa Allaah ambapo vinavyojulikana ni Tawraat, Zabuur, Injiyl, sahifa za Ibraahiym na Muusa na Qur-aan iliyoteremshwa kwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Qur-aan ndio yenye kuvidhibiti vyote.

Kuwaamini Mitume kuanzia wa mwanzo wao, ambaye alikuwa ni Nuuh, mpaka wa mwisho wao, ambaye alikuwa ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Inatakiwa kuamini kwamba ni wenye kutoka kwa Allaah. Allaah amewateua kwa ujumbe na ni wakatikati baina Yake na viumbe Wake. Vilevile inapasa kuamini kwamba Allaah amewatumiliza ili kufikisha hukumu za Shari´ah kwa waja Wake.

Allaah (Subhaanah) ametukhabarisha kwamba wako Mitume ambao ametusimulia khabari zao kupitia Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Mitume wengine hakutusimulia. Muhimu ni kwamba Mtume wa mwisho ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuamini Qadar kheri na shari yake ni kwamba kuamini kuwa Qadar ni yenye kutoka kwa Allaah na kwamba ameandika kila kitu kitachotokea. Kila kiumbe katika viumbe Allaah amekwishaandika kitapatikana sehemu fulani na katika wakati fulani na kama kiumbe hicho kitakuwa chenye kuamini au chenye kukufuru, chema au kiovu. Kila mtu anapata kile kilichoandikwa kwa ajili yake au dhidi yake.

Kuamini siku ya Mwisho ambapo Allaah atamlipa kila mmoja kwa kile alichokitenda.

Hii ndio imani na ni jina la imani ya matendo.

Imani inakusanya vilevile matendo ya viungo. Kusimama katika swalah, kurukuu, kusujudu, kusoma Qur-aan, Tashahhud na kusema ”Subhaan Allaah” yote hayo ni katika matendo ya imani. Aidha mja kufunga kwa kuacha matamanio yake kwa ajili ya Allaah (Ta´ala) kunaingia katika imani. Pia mja kuzuia viungo vyake kutokamana na kuzishambulia mali za watu ni katika imani. Mja kutembea kutoka nyumbani kwake kwenda msikitini ili kutekeleza vipindi vitano vya swalah ni katika imani. Mja kumwogopa Allaah (´Azza wa Jall) pindi anapotenda dhambi na kuyaacha kwake madhambi ni katika imani. Shaykh as-Sa´diy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Dini yote, misingi yake na matawi yake vinaingia katika imani.”

Kama tulivyopiga mifano. Allaah alimlipa thawabu mwanamke mzinzi wa wana wa israaiyl pindi alipomwona mbwa aliyekuwa na kiu ambapo akampa maji kwa kutoleza mtandio wake ndani ya maji Allaah akamsamehe kwa sababu hiyo[2].

Allaah alimlipa thawabu na kumsamehe yule bwana ambaye alikata tawi lililokuwa likiwaudhi watu wenye kupita maeneo hayo[3].

Kuswali kwa wingi na matendo mema mengine kunaifanya imani kuwa na nguvu zaidi na kukua.

Upande mwingine upumbaaji, uchache wa kujali, kutoyatilia umuhimu matendo ya dini yote hayo yanapelekea kuidhoofisha dini ya mja mpaka mwishowe anaangamia na habaki isipokuwa na kitu kichache. Kwa ajili hiyo ndio maana wanachuoni wakasema kuwa imani inazidi kwa matendo mema na inapungua kwa maasi. Matendo mema aina zote yanaifanya imani kupanda. Kuswali kwa njia inayotakikana kunaifanya imani kuzidi. Kusoma kunaifanya imani kuzidi. Kuyahifadhi masikio kutokamana na kusikiliza maneno duni kunaifanya imani kuzidi. Kuyahifadhi macho kutokamana na kuona vitu vya haramu kunaifanya imani kuzidi. Kuihifadhi mikono kutokamana na vile vyote alivyoharamisha Allaah kunaifanya imani ikapanda. Muumini hatakiwi kuwaibia wengine. Asiwapore wengine. Asiwahadae wengine na kadhalika. Mguu wa muumini hauendi katika maasi. Anatakiwa kujizuia kutokamana na hayo kwa ajili ya kumwamini Allaah. Yote hayo ni matendo yanayoifanya imani kuzidi. Hayohayo ndio yanayosemwa juu ya matendo mengine yote.

Yule mwenye kuamini kwamba imani ni kutamka kwa mdomo, kuamini ndani ya moyo na matendo ya viungo na kwamba inazidi kwa matendo mema na inashuka kwa maasi basi ametoka katika Irjaa´ na ´Aqiydah ya Murji-ah. Miongoni mwa dalili ya hayo inatutosha Hadiyth ya uombezi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kwamba Allaah atasema:

“Tazameni yule ambaye moyoni mwake mna imani sawa na uzito wa dinari mumwondoshe.”[4]

“Yule ambaye moyoni mwake mna imani sawa na uzito wa dinari mumwondoshe, kisha yule ambaye moyoni mwake mna imani sawa na nusu dinari mumwondoshe,  kisha yule ambaye moyoni mwake mna imani sawa na kokwa ya tende mumwondoshe, kisha yule ambaye moyoni mwake mna imani sawa na mduduchungu kisha yule ambaye moyoni mwake mna imani ndogo, ndogo na ndogo kabisa kuliko mduduchungu.”[5]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا

“Hakika Allaah hadhulumu uzito wa atomu. Na ikiwa ni [kitendo] kizuri hukizidisha na hutoa kutoka kwake ujira mkubwa.”[6]

[1] Muslim (8).

[2] al-Bukhaariy (3467) na Muslim (2245).

[3]  al-Bukhaariy (2472) na Muslim (1914).

[4] Ahmad (3/16) na al-Bukhaariy (7439).

[5] al-Bukhaariy (7439) na Muslim (183).

[6] 04:40

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 40-45
  • Imechapishwa: 29/09/2021