Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

20 – Amewaumba viumbe kwa ujuzi Wake.

21 – Amewakadiria makadirio yao.

22 – Ameshahukumu muda wao wa kuishi.

23 – Hakuna kilichofichikana Kwake kabla Yeye kuwaumba.

24 – Aliyajua yale watakayoyatenda kabla ya kuwaumba.

25 – Amewaamrisha kumtii Yeye na akawakataza kumuasi.

26 – Kila kitu kinapitika kwa makadirio na utashi Wake.

27 – Matakwa Yake ni yenye kutekelezeka. Hakuna waja wanachotaka isipokuwa kile Alichowatakia. Kile Anachowatakia, kinakuwa. Na kile Asichowatakia, hakiwi.

MAELEZO

Maana yake ni kwamba matakwa Yake Allaah (Ta´ala) ni yenye kuwaenea viumbe wote, ni mamoja ni cha kheri au cha shari, uongofu au upotevu. Zipo Aayah nyingi na zinazotambulika zinazofahamisha juu ya hilo.

Malengo ya nukta hizi ni kuwaraddi Mu´tazilah wanaopinga kuenea kwa matakwa ya Allaah (Ta´ala). Hata hivyo ni lazima kutambua kuwa kusema kuwa Allaah anakijua kila kinachotokea, haina maana kwamba Anakipenda kitokee. Mapenzi ni tofauti na matakwa. Vinginevyo Allaah (Ta´ala) asingelitofautisha kati ya mwema na muovu. ´Aqiydah hii imetamkwa waziwazi na baadhi ya wakuu wa Wahdat-ul-Wujuud, nayo ni kwamba mwema na muovu wote wawili ni wenye kumtii Allaah katika utashi Wake.

Salaf, wanazuoni na wengi katika Ahl-us-Sunnah na wengineo wanaothibitisha makadirio wanatofautisha kati ya matakwa na mapenzi ya Allaah. Hayo yametiliwa nguvu na mtunzi wa kitabu ”Bad´-ul-Amaaliy” pindi aliposema:

Ni Mwenye kutaka kheri na shari mbaya

lakini haridhii mambo yasiyowezekana

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Qadariyyah wanasema kuwa Allaah hapendi kufuru, dhambi na uasi na kwa ajili hiyo hataki mambo hayo yatokee. Kwa maana hiyo ni kwamba yale asiyoyataka, hutokea, na yale anayotaka, hayatokei.

Kundi lingine la Qadariyyah wanaothibitisha makadirio linasema kuwa yale anayotaka, hutokea, na yale asiyoyataka, hayatokei. Kwa maana hiyo ni kwamba ametaka kutokee kufuru, dhambi na uasi pasi na kutaka yatokee kwa mtazamo wa kidini, au ametaka yatokee kwa kafiri lakini hakutaka yatokee kwa muumini. Kwa msemo mwingine ni kwamba anapenda kufuru, dhambi na uasi na wala hayapendi kwa mtazamo wa kidini, na kwamba anayapenda kutoka kwa kafiri na wala hayapendi kutoka kwa muumini.

Nadharia zote mbili ni za kimakosa na zinapingana na Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf na maimamu wa ummah. Kwani wote wameafikiana juu ya kwamba yale ambayo Allaah hutaka kutokea, yanatokea, na yale ambayo Allaah hataki yotokee, hayatokei, na kwamba hakutokei jambo lolote isipokuwa kwa kutaka Kwake na kwamba hapendi maharibifu na wala haridhii kufuru kutoka kwa waja Wake. Amesema kuhusu makafiri:

يَسْتَخْفُونَ مِنَ النَّاسِ وَلَا يَسْتَخْفُونَ مِنَ اللَّـهِ وَهُوَ مَعَهُمْ إِذْ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرْضَىٰ مِنَ الْقَوْلِ

”Wanajificha watu wasiwaone na wala hawajifichi kwa Allaah ilihali yupamoja nao pale wanapokesha kupanga njama kwa maneno asiyoyaridhia.”[1]

[1] 04:108

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 15/09/2024