Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

28 – Anamwongoza amtakaye. Analinda na kuafu kutokana na fadhilah. Anapotosha, anakosesha nusura na kujaribu kwa uadilifu.

29 – Wote wanaendeshwa na matakwa ya Allaah, baina ya fadhilah Zake na uadilifu Wake.

30 – Ametakasika kutokamana na wapinzani na washirika.

31 – Hakuna yeyote awezaye kurudisha nyuma mipango Yake, kupinga hukumu Yake wala kushinda amri Yake.

32 – Tumeyaamini yote hayo na tumeyakinisha kuwa yote ni yenye kutoka Kwake.

33 – Muhammad ni mja Wake aliyeteuliwa, Nabii Wake aliyechaguliwa na Mtume Wake aliyeridhiwa.

MAELEZO

Tambua kuwa kila Mtume ni Nabii na si kila Nabii ni Mtume. Kumetajwa tofauti nyingi kati ya Mtume na Nabii, jambo ambalo unaweza kulipata katika ”Ruuh-ul-Ma´aaniy” (5/449-450) ya al-´Aaluusiy. Maoni yaliyo karibu zaidi na usahihi ni kwamba Mtume ni yule aliyetumilizwa kwa Shari´ah mpya na Nabii ni yule ambaye ametumilizwa kuthibitisha Shari´ah iliokuwa kabla yake. Hapana shaka yoyote Nabii pia ameamrishwa kufikisha Shari´ah hiyo. Ni jambo linalotambulika kuwa wanazuoni wameamrishwa kufanya hivo, kwa hivyo inatambulika kuwa Manabii watakuwa na haki zaidi ya kufanya hivo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 15/09/2024