07. Maafikiano ya Ahl-ul-Hadiyth kuhusu Allaah kuwepo juu ya mbingu

Ahl-ul-Hadiyth wanaitakidi na kushuhudia ya kwamba Allaah (Subhaanah) yuko juu ya mbingu ya saba na amelingana juu ya ´Arshi Yake, kama Alivotamka Mwenyewe ndani ya Kitabu Chake:

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ‘Arshi; Anaendesha mambo yote.”[1]

اللَّـهُ الَّذِي رَفَعَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Allaah Ambaye ameinua mbingu bila ya nguzo mnaziona kisha akalingana juu ya ‘Arshi.”[2]

الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ الرَّحْمَـٰنُ

”Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, kisha akalingana juu ya ‘Arshi; Mwingi wa rehema!”[3]

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi.”[4]

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

“Yeye Ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ‘Arshi. Anajua yale yanayoingia ardhini na yale yatokayo humo na yale yanayoteremka kutoka mbinguni na yale yanayopanda humo – Naye yupamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah ni Mwenye kuona yote myafanyayo.”[5]

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ

“Kwake pekee linapanda neno zuri na kitendo hukitukuza.”[6]

يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مِنَ السَّمَاءِ إِلَى الْأَرْضِ ثُمَّ يَعْرُجُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ أَلْفَ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ

”Anaendesha mambo kutoka mbinguni mpaka ardhini, kisha inapanda Kwake katika siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu katika ile mnayoihesabu nyinyi.”[7]

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ

“Je, mnadhani mko katika amani na aliyeko juu mbinguni kwamba hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika?”[8]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameeleza kuwa Fir´awn aliyelaaniwa alimwambia Haamaan:

يَا هَامَانُ ابْنِ لِي صَرْحًا لَّعَلِّي أَبْلُغُ الْأَسْبَابَ أَسْبَابَ السَّمَاوَاتِ فَأَطَّلِعَ إِلَىٰ إِلَـٰهِ مُوسَىٰ وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ كَاذِبًا

“Ee Haamaan! Nijengee mnara ili nifikie njia. Njia za mbinguni ili nimchungulie Mungu wa Muusa, kwani hakika mimi namdhania ni mwongo.”[9]

Alisema hivo kwa sababu alimsikia Muusa (´alayhis-Salaam) akitaja kuwa Mola wake yuko juu ya mbingu. Huoni amesema:

وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ كَاذِبًا

”… kwani hakika mimi namdhania ni mwongo.”?

Bi maana anaposema kuwa kuna mungu juu ya mbingu.

Wanazuoni wa ummah na maimamu wa Salaf (Rahimahumu Allaah) hawakuwahi kukhitilafiana juu ya kwamba Allaah (Ta´ala) yuko juu ya ´Arshi Yake na kwamba ´Arshi Yake iko juu ya mbingu Zake. Wanamthibitishia yale ambayo Allaah (Ta´ala) amejithibitishia Mwenyewe. Wanayaamini na wanamsadikisha Mola (Jalla Jallaaluh) katika maneno Yake. Wanasema yaleyale Aliyosema (Subhaanahu wa Ta´ala) kuhusu kulingana Kwake juu ya ´Arshi, wanayapitisha katika udhahiri wake na wanamtegemezea ujuzi Wake Allaah. Wamesema:

آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ

”Tumeziamini; zote ni kutoka kwa Mola wetu, na hawakumbuki isipokuwa wale wenye akili.”[10]

Allaah (Ta´ala) ameeleza kuwa wale waliobobea katika elimu husema hivo. Allaah akaridhika nao na akawasifu kwa hilo.

[1] 10:3

[2] 13:2

[3] 25:59

[4] 7:54

[5] 57:4

[6] 35:10

[7] 32:05

[8] 67:16

[9] 40:36-37

[10] 3:7

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 175-176
  • Imechapishwa: 04/12/2023