Kuna uombezi ambao ni haki na ambao ni batili. Uombezi ambao ni haki na sahihi ni ule uliotimiza sharti mbili:

1 – Uwe kwa idhini ya Allaah.

2 – Yule anayeombewa awe ni katika wapwekeshaji, yaani katika watenda dhambi wanaomwabudu Allaah pekee.

Kukikosekana sharti moja katika sharti hizi mbili, basi uombezi unakuwa batili. Amesema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?” (02:255)

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“Na wala hawamuombei uombezi yeyote yule isipokuwa yule Anayemridhia.” (21:28)

Hawa wenye kuombewa ni watenda dhambi wapwekeshaji. Kuhusu makafiri na washirikina, hautowafaa kitu uombezi wa waombezi:

مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ

“Madhalimu hawatokuwa na rafiki na wala mwombezi anayetiiwa.” (40:18)

Watu hawa wamesikia kunazungumzwa kuhusu uombezi na wala hawakujua maana yake. Kwa ajili hiyo ndio wakaanza kuwaomba wafu uombezi bila ya idhini ya Allaah (´Azza wa Jall). Wameuomba vilevile kutoka kwa washirikina ambao wao wenyewe hautowafaa kitu uombezi wa waombezi. Watu hawa ni wajinga juu ya uombezi sahihi na vivyo hivyo uombezi batili. Kwa hivyo uombezi una sharti na haukuachwa hivihivi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 20-21
  • Imechapishwa: 18/08/2022