07. Hadiyth “Uislamu umejengwa juu ya mambo matano… ”

´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kuwa hakuna wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kuhiji Nyumba na kufunga Ramadhaan.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hii Hadiyth ni dalili ya kwamba hajj ni waajibu na kwamba ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu kwa yule anayeweza kuifikia. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

”Kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo wa kuiendea. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni mkwasi kwa walimwengu.”[2]

Miongoni mwa fadhilah, rehema Yake na wepesi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni kwamba Hajj imefaradhishwa mara moja tu katika maisha. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hajj ni mara moja, basi atakayezidisha basi hiyo ni ya kujitolea.”[3]

Wameipokea watunzi wa Sunan isipokuwa tu at-Tirmidhiy na cheni yake ni Swahiyh.

Ni lazima kwa muislamu kuharakia kufanya Hajj mara tu masharti yatakapotimia na vizuizi kuondoka, kwa sababu haijulikani ni nini kinaweza kumzukia baadae. Imepokewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas au kutoka kwa al-Fadhwl au mmoja wao kutoka kwa mwenzake, ambaye amesimulai kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanyeni haraka katika Hajj… ”

Kwa maana ya hajj ya faradhi

”… kwa sababu hakuna yeyote katika nyinyi ambaye anajua litakalompata.”[4]

Ameipokea Ahmad.

[1] al-Bukhaariy (08) na Muslim (16).

[2] 03:97

[3] Abu Daawuud (1721), an-Nasaa’iy (05/111), Ibn Maajah (2886) na Ahmad (05/331) kupitia kwa Ibn Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Hadiyth ni Swahiyh na asili yake ni kwa Muslim (1337) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] Ahmad (01/314) na ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa´-ul-Ghaliyl” (4/168). Tazama ”Idhwaa´ul-Bayaan” (05/115).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 05/05/2025