07. Fadhilah za kuomuombea du´aa nduguyo nyuma ya mgongo wake

37 – Abu Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakuna muislamu anayemuombea du´aa ndugu yake nyuma ya mgongo wake isipokuwa Malaika husema: “Nawe upewe mfano wake.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Du´aa ya muislamu kumuombea ndugu yake nyuma ya mgongo wake ni yenye kuitikiwa. Karibu na kichwa chake kuna Malaika aliyepewa kazi ambaye kila anapomuombea du´aa ndugu yake jambo la kheri, Malaika huyo aliyepewa kazi husema: “Aamiyn, nawe upewe mfano wake.”[1]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Hadiyth inafahamisha ubora wa muislamu kumuombea du´aa ndugu yake nyuma ya mgongo wake. Kwa maana nyingine akiwa mbali naye. Du´aa hiyo ni yenye kuitikiwa.

Hadiyth inajulisha pia kuwa ananufaika yule mwombaji na yule mwombewaji, kwa sababu Malaika huitikia “Aamiyn” juu ya du´aa ya mwombaji kwa kusema “Nawe upewe mfano wake”. Hivyo anapewa mfano wa yale aliyomuombea ndugu yake nyuma ya mgongo wake.

[1] Muslim (2732) na (2733).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 41
  • Imechapishwa: 08/10/2025