07. Baadhi ya sifa za Pepo na wakazi wake

05 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) anasema: “Nimewaandalia waja Wangu wema yale ambayo hajaonwa na jicho lolote, hayajasikiwa na sikio lolote na wala hayajapita kwenye moyo wa yeyote.” Mkitaka someni:

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاء بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Hakuna yeyote anayejua yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho yakiwa ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[1][2]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inafahamisha juu ya malipo makubwa na neema zenye kudumu ambazo Allaah (Ta´ala) amewaandalia waja Wake wema kwa ajili ya kuwahurumia na kuwalipa juu ya matendo yao. Neema hizi hakuna anayejua uzuri wazo na kiwango chake isipokuwa Allaah (Ta´ala). Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Zingatia jinsi alivyokabili kusimama kwao usiku kwa malipo ambayo amewafichia ambayo hakuna nafsi yoyote inayajua na jinsi alivyokabili mahangaiko na kusumbuka kwao juu ya vitanda vyao wakati wanaposimama usiku kuswali kwa wanawake wa Peponi.”[3]

Zipo Aayah na Hadiyth nyingi sana zilizotaja sifa za Peponi na neema zake na sifa za wakazi wake. Amesema (Ta´ala):

وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ۖ وَأَنتُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

”… na humo mna yale zinazotamani nafsi na ya kuburudisha macho, nanyi humo ni wenye kudumu.”[4]

وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Wape bishara njema wale walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo chini yake mito, kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni riziki husema “Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla” na wataletewa hali ya kuwa yanafanana; na watapata humo wake waliotwahirika nao humo ni wenye kudumu milele.”[5]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kundi la kwanza litakaloingia Peponi umbo lao litakuwa kama umbo la mwezi unapokuwa kamili. Hawatotema mate, hawatotokwa na kamasi na wala hawatoi haja kubwa humo. Vyombo vyao vinatokana na dhahabu. Vitana vyao ni vya dhahabu na fedha, vyetezo vyao watatumia ni udi wa mawardi, jasho lao linanukia miski. Kila mmoja katika wao atakuwa na wake wawili. Kilichoko ndani ya miguu yao kitaonekana nyuma ya ngozi yao kutokana na uzuri. Hakutokuwa mizozo wala kuchukiana; mioyo yao ni kama umbo la mtu mmoja. Wanamsabihi Allaah asubuhi na jioni.”[6]

Burudisho bora kabisa analopata mtu Peponi ni kumuona Allaah (Ta´ala). Jariyr (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Tulikuwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akautazama mwezi usiku wa mwezi mng´aro kisha akasema: “Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi huu. Hamtosongamana katika kumtazama. Mkiweza kutoshindwa kuswali kabla ya jua kuchomoza na kabla ya kuzama kwake, basi fanyeni. Kisha akasoma:

وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا

“… na tukuza kwa himdi za Mola wako kabla ya kuchomoza jua na kabla kuzama kwake.”[7][8]

Neema za Peponi ni zaidi ya maelezo na fikira zinafupika kuziwaza. Watendaji wanastahiki kabisa kuzifanyia kazi na kushindana wale wenye kushindana. Hivi ndio ilikuwa hali ya Salaf wa ummah huu. Kisha baada yao wakaja watu ambao wakageuza mambo ambapo wakawa wanashindana kuikusanya dunia. al-Hasan amesema:

“Ukiwakuta watu wanafanya kheri basi shindana nao, na ukiwakuta katika maangamivu basi waache na kile walichokichagua.”

Ni lazima kwa muislamu atamani zile neema za milele alizoziandaa Allaah na muda wa kuishi kwake ajitahidi kufanya matendo mema na ahakikishe yuko na zile sifa za watu wa Peponi ambazo Allaah amezitaja ndani ya Qur-aan na Sunnah kukiwemo kumuamini Allaah (Ta´ala) na kila ambacho mtu analazimika kukiamini, kulazimiana na kumcha, kunyooka katika kumtii, kupupia aina mbalimbali za ´ibaadah, ajipambe kwa tabia tukufu kukiwemo kutenda wema, kusamehe, kutoangalia vitu vya haramu, kujiepusha na upuuzi, vikao vya uwongo, kuhifadhi tupu kutokana na vile alivyoharamisha Allaah na mengineyo.

[1] 32:17

[2] al-Bukhaariy (3244) na Muslim (2824).

[3] Haadiy al-Arwaah, uk. 174.

[4] 43:71

[5] 02:25

[6] al-Bukhaariy (3245).

[7] 20:130

[8] al-Bukhaariy (554) na Muslim (633).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 70-72
  • Imechapishwa: 05/03/2023