Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

19 – Kwa sababu Yeye juu ya kila jambo ni muweza. Kila kitu ni chenye kumuhitajia Yeye. Kila jambo Kwake ni jepesi:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

MAELEZO

Baadhi wanasema kuwa Allaah ni muweza kwa yale Anayoyataka. Hayo si sahihi. Sahihi ni yale yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah; kwamba Yeye juu ya kila kitu ni muweza kwa sababu matakwa na uwezo Wake ni vyenye kuenea.

Mu´tazilah wanasema kuwa Allaah (Ta´ala) hakutaka mja aingie ndani ya madhambi; bali mja mwenyewe ndiye kataka hivo, na si Allaah. Kwa ajili hiyo amesema mmoja katika wapotofu wao:

Amedai mjinga na yule mwenye kuonelea kama yeye

ya kwamba Muumba ndiye kahukumu maasi

ikiwa hayo anayoyasema ni kweli

ni kwa nini basi aadhibiwe mzinzi na mwizi akatwe mkono?

Abul-Khattwaab (Rahimahu Allaah) amesema pindi alipokuwa akibainisha haki na usawa:

Wamesema: “Vipi basi matendo ya waja?”

Nikasema hakuna Muumba isipokuwa Mungu mtukufu

Wakasema: “Je, anataka kutokee kwa mambo mabaya?”

Nikasema matakwa yote yanayokana na Mola

Ni upungufu ikiwa yatatokea pasi na kutaka Kwake

Ametakasika kushindwa na kitu duni

Matakwa anayozungumzia Abul-Khattwaab ni ya kilimwengu, na si ya kidini. Hayo atakuja kubainishwa huko mbele.

[1] 42:11

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad bin ´Abdil-´Aziyz bin Maaniy´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haashiyah ´alaa al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 11/11/2021