07. Aina za watu wanaokufa na hukumu ya kuwatembelea

Swali: Tunaona umakini wako mkubwa katika suala la kuyatembelea makaburi na kutafuta baraka kwa wale waliyomo ndani yake katika watu wema. Hapana shaka yoyote ya kwamba wako na kheri nyingi kwa kuzingatia kwamba wanaishi katika mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Isitoshe wao wako karibu zaidi na Allaah kuliko wengine. Kwa sababu wao wako mbele Yake. Lakini kule kuzungumza kwako kwa wingi juu ya kutokuwa kwao na faida kumetufanya tuweke maswali mengi pale tunapotaka kuwatembelea watu hawa. Kwa hiyo tunaomba kutoka kwenu utusadikishe maneno yetu – Allaah atuwafikishe sisi na nyinyi. Kwa sababu kama hatuko katika usawa basi tunataka kujiepusha na yale tunayofanya hivi sasa.

Jibu: Muulizaji ni mwenye kushukuriwa kwa kule kuitafuta kwake haki. Hilo ndilo linalompasa kila muumini aulize juu ya yale yanayomtatiza na wala asibaki juu ya ujinga. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Hivyo basi waulizeni watu wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.”[1]

Waliokufa ndani ya makaburi wako aina mbalimbali:

1 – Miongoni mwao wako ambao wako karibu na Allaah na chini ya ulinganizi wa Allaah ni wenye kurehemewa. Hawa ni wale wenye kumcha Allaah na wenye imani.

2 – Miongoni mwao wako walioghadhibikiwa ambao ni makafiri na watenda maasi mazito.

Watu aina mbizi hizi hawalingani.

Muumini mzuri ambaye amekufa juu ya kumtii Allaah na Mtume Wake yuko katika kheri kubwa na ameahidiwa Pepo na pia kaburi lake ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi.

Kuhusu wale waliokufa juu ya kumkufuru Allaah kama wale ambao wanawaomba waliokufa, wanataka uokozi na msaada waliokufa, huu ni ukafiri na upotofu. Huyu yumo katika khatari kubwa. Ameahidiwa Moto na adhabu yenye kuumiza kwa kumkufuru na kumshirikisha kwake Allaah.

Vivyo hivyo yule aliyekufa juu ya maasi pasi na kutubia. Kama mfano wa yule ambaye amekufa juu ya uzinzi, utovu wa nidhamu kwa wazazi wawili, ulaji ribaa, kushuhudia uongo, unywaji pombe, kuiba pesa za watu na mfano wa hayo. Hawa wako katiak khatari kubwa ya kuingia Motoni na kuna khatari makaburi yao yakawa ni shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni. Kwa hivyo kifo hakilingani.

Kwa hivyo, muulizaji, unapaswa kutambua kwamba wafu wako sampuli mbalimbali. Miongoni mwao wako ambao wameridhiwa na wamenyooka sawasawa ambao wamekufa juu ya kumcha Allaah na kumwamini. Hawa ni wenye kupata Pepo na heshima na makaburi yao ni mabustani miogoni mwa mabustani ya Peponi. Wengine wamekufa juu ya ukafiri na upotofu kama mfano wa wale wenye kuichezea shere dini, kuitukana dini, wakaacha swalah, wakawaomba wafu, wakawataka uokozi na msaada na mfano wa hayo. Huku ni kumkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Makafiri ni wenye kuahidiwa Moto wakifa juu ya ukafiri wao. Wako pia waislamu ambao wamekufa juu ya maasi kama mfano wa wale ambao wamekufa juu ya kunywa pombe, ribaa, uzinzi, wizi au wamekufa juu ya kuwaasi wazazi wawili. Hawa wako katika khatari kubwa. Ijapo hata wakiingizwa ndani ya Moto hawatodumishwa humo milele. Hata hivyo wako katika khatarini na wako katika khatari ya kuadhibiwa ndani ya kaburi kwa sababu ya maasi yao.

Kuhusu kuyatembelea makaburi kumegawanyika aina mbalimbali. Wakiwa ni waislamu basi wanatembelewa kwa ajili ya kuwaombea du´aa, kuwatakia rehema, kuwaombea msamaha, kukumbuka Aakhirah na kuipa kisogo dunia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwafunza Maswahabah zake pindi wanapoyetembelea makaburi waseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية يرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya. Allaah amrehemu aliyetangulia katika sisi na atakayekuja baadaye.”[2]

Pia alikuwa akisema:

اللهم اغفر لأهل بقيع الغرقد

Ee Allaah! Wasamehe watu wa al-Baqiy´ al-Gharqad.”[3]

Kwa hivyo ukiwatembelea waombee kwa Allaah msamaha, rehema na afya. Ama kuwaomba wakukidhie mahitaji yako, wakuponyee wagonjwa wako na mahitaji mengine ni kumshirikisha Allaah na haijuzu. Matendo haya ni ya kipindi kabla ya kuja  Uislamu na ni miongoni mwa matendo ya Abu Jahl, makafiri wengine wa kipindi kabla ya kuja  Uislamu, makafiri wengine wa ki-Quraysh na mfano wao. Wafu hawaombwi kitu; hawaombwi uokozi, nusura wala kuponyesha wagonjwa. Haya yanaombwa kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na si kutoka kwao. Yeye ndiye Muweza wa kila kitu (Subhaanahu wa Ta´ala). Wafu hawaombwi uombezi. Wanaombewa msamaha, wakaombewa du´aa na rehema. Unapaswa kuyajua hayo na uwe juu ya ubainifu.

Kuhusu makafiri – kama vile wakristo – hawatembelewi. Makaburi ya mayahudi, makaburi ya manaswara na makaburi ya washirikina ambao wanamwabudu asiyekuwa Allaah, wanawaomba uokozi waliokufa na kuwawekea nadhiri, hawa hayatembelewi makaburi yao. Yule anayewatembelea kwa lengo la mazingatio hapana vibaya akiwatembelea kwa lengo la mazingatio. Nakusudia lengo likiwa mazingatio na kukumbuka Aakhirah. Lakini asiwaombee du´aa na kuwatakia rehema.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilitembelea kaburi la mama yake ambaye alikufa juu ya kipindi cha kishirikina. Alitembelea kaburi la mama yake na akamwomba Mola Wake amwombee msamaha. Lakini hata hivyo hakumpa idhini amwombee msamaha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alilitembelea kwa ajili ya mazingatio na makumbusho peke yake. Hapana vibaya akiyatembelea makaburi ya makafiri katika manaswara na wengineo kwa minajili ya makumbusho, mazingatio, kuipa nyongo dunia na shauku juu ya Aakhirah. Lakini asiwatolee salamu na wala asiwaombee du´aa.

Kuhusu waislamu yanatembelewa makaburi yao na wanaombewa du´aa ya msamaha na rehema. Hawaombwi pamoja na Allaah, hawatakwi uokozi, hawawekewi nadhiri, hawaombwi uombezi, uokozi wala nusura. Yote haya hayajuzu. Yote haya ni shirki iliyoharamishwa na Allaah. Isitoshe ni miongoni mwa matendo ya watu wa kipindi cha kishirikina.

Kwa hivyo, muulizaji, unatakiwa uyahifadhi haya vizuri na uwafikishie walioko pambizoni mwako katika majirani zako na marafiki zako ili muwe juu ya utambuzi. Kwa sababu Allaah amesema:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[4]

Wafu na vivyo hivyo Malaika na Mitume hawaombwi baada ya kufa kwao. Hali kadhalika nyota, miti, mawe na masanamu vyote hivi haviombwi badala ya Allaah, haviombwi uokozi, haviwekewi nadhiri na wala havipapaswi. Kuhusu Nabii akiwa hai na mja mwema ambaye anasikia maneno yako hapana vibaya kumwambia akuombee kwa Allaah, ni kama ambavo Maswahabah katika uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakimwomba Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awaombee. Haya walikuwa wakiyafanya katika uhai wake kabla ya kufariki kwake. Maswahabah walikuwa wakimwomba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) du´aa na uombezi. Ama baada ya kufa hapana. Namna hii mtu mwema katika ndugu zako; mtu aliyeshikamana na swalah na ´ibaadah nyenginezo ukamuomba akuombee kwa Allaah na wakati huohuo anasikia maneno ya waliohai ambapo ukamuomba akuombee kwa Allaah msamaha na akutengenezee hali na dhuriya yako hapana vibaya.

Kinacholengwa ni kwamba hapana neno kumwomba aliye hai na muweza yale anayoyaweza. Kwa mfano ukamwomba akuombee du´aa, akukopeshe sehemu ya mali yake kutokana na mahitaji yako na kushirikiana katika kitu. Hapana vibaya kwa mambo haya yanayokuwa kati yako na yule aliye hai, mbele yako na muweza. Kuhusu wafu hawaombwi kitu, hawaulizwi na wala hawatakwi uokozi. Vivyo hivyo vile viumbe visivyokuwa na uhai kama mfano wa majibali, masanamu, nyota na mfano wake. Viumbe kama hivi haviombwi na wala havitakwi uokozi. Hali kadhalika viumbe visivyoonekana katika majini na Malaika haifai kuwaomba na kuwataka uokozi. Yote haya ni kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Mwombe Mola Wako mahitaji yako; mwombe (Subhaanah) amponye mgonjwa wako, akunusuru dhidi ya maadui zako na umwombe msaada kutoka katika fadhilah Zake kwa msaada, uwafikishwaji na uwongofu. Yote haya yanaombwa kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] 16:43

[2] Muslim (974).

[3] Muslim (974).

[4] 72:18

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 32-38
  • Imechapishwa: 12/04/2022