Mlinganizi anatakiwa awe mwenye subira juu ya ulinganizi wake, awe mwenye subira kwa yale anayolingania kwayo, awe na subira kwa yale yanayokwamisha ulinganizi wake na awe na subira kwa yale maudhi yanayompata. Mlinganizi anapaswa kuwa na subira juu ya ulinganizi na mvumilivu juu yake na asiikatishe wala isimchoshe. Bali anatakiwa awe mwenye kuendelea kulingania kwa Allaah kwa kiasi cha uwezo wake na katika yale maeneo ambayo ulinganizi unakuwa wenye manufaa, bora na mafanikio zaidi. Asubiri juu ya ulinganizi wake na wala asichoke. Mtu akizidiwa na machovu basi huchoka na akaacha. Lakini akiwa mvumilivu juu ya ulinganizi wake basi mosi hupata ujira wa wenye kusubiri na pili hupata mwisho mwema. Sikiliza maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) akimzungumzisha Mtume Wake:

تِلْكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهَا إِلَيْكَ ۖ مَا كُنتَ تَعْلَمُهَا أَنتَ وَلَا قَوْمُكَ مِن قَبْلِ هَـٰذَا ۖ فَاصْبِرْ ۖ إِنَّ الْعَاقِبَةَ لِلْمُتَّقِينَ

“Hizo ni katika khabari zilizofichikana Tunazokufunulia Wahy. Hukuwa unazijua wewe na wala watu wako kabla ya hii [Qur-aan]. Basi subiri, hakika mwisho mwema ni kwa wenye kumcha Allaah.”[1]

Ni lazima kwa mtu awe mwenye kuvumilia vile vipingamizi na malumbano yanayokumba ulinganizi wake. Kila mtu anayelingania kwa Allaah basi ni lazima apingwe:

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ ۗ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ هَادِيًا وَنَصِيرًا

“Hivyo ndivyo Tumemfanyia kila Nabii kuwa na adui miongoni mwa wakhalifu – na Mola wako anatosheleza kuwa ni Mwenye kuongoza na Mwenye kunusuru.”[2]

Kila ulinganizi wa haki ni lazima upate upinzani. Ni lazima ipate vizuizi, pingamizi na wakosoaji. Lakini ni lazima kwa mlinganizi kufanya subira juu ya yale yanayokumba ulinganizi wake. Hata kama ulinganizi wake utaelezwa kuwa wa makosa na wa batili ilihali yeye anatambua kuwa ndivo inavyopelekea Qur-aan na Sunnah basi awe mvumilivu juu ya hilo.

Lakini haina maana kwamba mtu aendelee kung´ang´ania juu ya yale anayoyasema na yale anayolingania ijapokuwa itambainikia haki. Ambaye anaendelea kushikilia yale anayolingania kwayo, ijapo haki imembainikia, amefanana na wale ambao Allaah amesema juu yao:

يُجَادِلُونَكَ فِي الْحَقِّ بَعْدَ مَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى الْمَوْتِ وَهُمْ يَنظُرُونَ

“Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika, kama kwamba wanasukumwa katika mauti nao huku wanatazama.”[3]

Kubishana baada ya kuwa haki imekwishabainika ni sifa inayosimangwa. Allaah amesema juu ya wale wenye kusifika na sifa hiyo:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

”Yule atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na ni uovu ulioje mahali pa kuishia!”[4]

Vile vikwazo vitavyotokea ulinganizi wako, ikiwa ni haki, basi ni lazima kwako kuirejea, na ikiwa ni batili, basi kusifanye azimio lako la kuendelea mbele na ulinganizi wako.

[1] 11:49

[2] 25:31

[3] 08:06

[4] 04:115

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 14
  • Imechapishwa: 01/11/2021