06. Vipi usahihi wa Uislamu wa anayekiri shahaadah lakini hafanyi matendo yoyote?

Swali 6: Ni ipi hukumu ya mtu anayeyaacha kabisa matendo yote ya dhahiri ilihali anakiri shahaadah na anakiri faradhi, lakini hafanyi chochote kabisa? Je, mtu huyu ni muislamu pamoja na kuzingatia pia kwamba hana udhuru wowote unaokubalika katika Shari´ah unaomzuia kutekeleza faradhi hizo?

Jibu: Mtu huyu si muumini. Anayedai kuwa ni mwenye kusadikisha moyoni mwake lakini haonyeshi hilo kwa ulimi wake wala kwa matendo yake, basi imani yake haithibiti. Hii ni imani kama imani ya Ibliys na ya Fir´awn, kwani hata Ibliys alisadikisha moyoni mwake. Amesema (Ta´ala):

قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ

”Akasema: ”Mola wangu! Basi Nipe muhula mpaka siku watakayofufuliwa.”[1]

Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Fir´awn na wafuasi wake:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا

“Wakazipinga kwa dhuluma na majivuno na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha.”[2]

Hivyo basi imani na usadikishaji wa moyoni lazima uthibitishwe kwa matendo. Lazima uthibitishwe kwa kutamka kwa ulimi na lazima uthibitishwe kwa vitendo. Ni lazima kusadikisha na kunyenyekea. Ikiwa moyo wake umenyenyekea kwa imani, basi viungo lazima vifanye kazi. Lakini mtu kudai tu kuwa amesadikisha moyoni mwake lakini hasemi shahaadah kwa ulimi wake na hafanyi matendo kwa viungo vyake, ilihali ana uwezo wa kufanya hivyo, basi imani iko wapi? Kama usadikishaji wake ungekuwa kamili na anayo nia safi, basi angefanya matendo. Lazima kuwe na matendo yanayothibitisha usadikishaji na imani hiyo. Dalili nyingi za Qur-aan na Sunnah zimekuja kuthibitisha hilo.

Vilevile mtu anayefanya matendo kwa viungo vyake – anaswali, anafunga na anahiji – matendo haya lazima yawe na imani ya ndani na usadikishaji unaoyahakiki. Vinginevyo yatakuwa kama Uislamu wa wanafiki ambao walikuwa wakiswali na hata wakipigana jihaad pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini hawakuwa waumini wa kweli kwa sababu hawakuwa na imani na usadikishaji wa kweli unaothibitisha matendo yao. Hivyo ni lazima kupatikane mambo mawili ili isihi imani.

1 – Usadikishaji wa ndani unaothibitishwa na matendo.

2 – Matendo ya nje yanayothibitishwa na usadikishaji wa moyoni.

Lakini ikiwa kuna usadikishaji wa ndani bila matendo, basi ni wapi uthibitisho wake? Kipi kinachothibitisha hilo na unyenyekevu?

Haiwezekani kuwe na usadikishaji wa kweli ambapo mtu huyo haswali na wala hatamki shahaadah ilihali anajua thawabu kubwa ambazo Allaah kawaandalia wanaotamka shahaadah na wanaoswali, na adhabu kali waliyoandaliwa wanaoacha swalah. Kama usadikishaji wake ungekuwa sahihi na imani yake kweli, basi ingemsukuma kufanya matendo. Kama angelikuwa na usadikishaji na imani sahihi basi vingechoma shubuha na matamanio. Kuacha swalah kunatokana shubuha na maasi yanatokana na matamanio na hivyo imani ya kweli huchoma shubuha na matamanio haya. Hii inathibitisha kuwa moyo wake hauna imani sahihi, bali ni maneno tu ya mdomo yasiyoathiri matendo. Vinginevyo kama mtu ana usadikishaji moyoni mwake lakini au kukubali moyoni mwake tu na asitamke kwa ulimi, maneno ya moyo hayakuvuka kwenda katika matendo ya moyo na katika unyenyekevu. Tunachotaka kusema ni kwamba yule anayedai kuwa anaamini moyoni mwake na hafanyi matendo kwa viungo vyake vya mwili, hii ndiyo ´Aqiydah ya Jahmiyyah. Kwa sababu hiyo Shaykh-ul-Islam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ni vigumu kutofautisha kati ya maarifa tu ya moyo na usadikishaji wa kweli usioambatana na matendo ya viungo.”

Anachotaka kusema ni kwamba ni kwamba hiyo ndio ´Aqiydah ya Jahmiyyah. Tunamuomba Allaah usalama.

Hivyo basi yule anayedai kuwa ni muumini lakini hatamki shahaadah kwa ulimi wake wala hafanyi matendo kwa viungo vyake, ilihali ana uwezo wa kufanya hivyo, basi hiyo ndio ´Aqiydah ya Jahmiyyah. Tunaomba Allaah hifadhi. Ni lazima kuwe na matendo yanayothibitisha usadikishaji huo, kama vile mtu anayefanya matendo naye lazima awe na usadikishaji na imani kwa ndani inayoyathibitisha.

[1] 38:79

[2] 27:14

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah wa Ajwibah fiy-Iymaan wal-Kufr, uk. 21-23
  • Imechapishwa: 01/01/2026