06. Sifa za Allaah ni kwa njia ya kuthibitisha na kukanushwa

2 – Kipengele cha pili: Sifa za Allaah zimegawanyika aina mbili:

1 – Zilizothibitishwa (Thubuutiyyah).

2 – Zilizokanushwa (Salbiyyah).

Zinazothibitishwa ni zile ambazo Allaah amejithibitishia nazo. Mfano wa sifa hizo ni uhai, ujuzi na uwezo. Ni lazima kumthibitishia nazo Allaah kwa njia inayomstahikia. Allaah ndiye ambaye amejithibitishia nazo na Yeye ni mtambuzi zaidi wa sifa Zake.

Zilizokanushwa ni zile ambazo Allaah amejikanushia nazo. Mfano wa sifa hizo ni kudhulumu. Hivyo inalazimika kumkanushia nazo Allaah kwa sababu Allaah amejikanushia nazo. Lakini ni lazima kwa mtu aamini kumthibitishia Allaah kinyume chake kwa njia kamilifu zaidi. Kukanusha hakukuwi kamili mpaka ndani yake kuwemo na jambo la kuthibitisha. Mfano wa hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا

“Na Mola wako Hamdhulumu yeyote.”[1]

Kwa hivyo ni lazima kumkanushia Allaah kudhulumu sambamba na kuamini kuthibiti uadilifu kwa Allaah kwa njia kamilifu zaidi.

[1] 18:49

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 25
  • Imechapishwa: 09/10/2022