06. Mtume alikubali swalah ya Tarawiyh iswaliwe mkusanyiko

Leo hakuna mtu wa Sunnah, ambaye ni mjuzi wa Sunnah, ambaye anatilia shaka kwamba swalah ya usiku, ambayo pia inatambulika kama swalah ya Tarawiyh, imewekwa katika Shari´ah kuiswali kwa mkusanyiko katika Ramadhaan, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikubali iswaliwe kwa mkusanyiko, yeye mwenyewe aliiswali na akabainisha fadhilah zake.

Inapokuja kuhusu kukubali kwake, Tha´labah bin Abiy Maalik al-Quradhwiy ameeleza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka usiku mmoja katika Ramadhaan na akawaona watu wanaswali pembezoni na msikiti. Akauliza: “Wanafanya nini watu hawa?” Mtu mmoja akajibu: “Ee Mtume wa Allaah, hawa ni watu hawajui Qur-aan sana, hivyo Ubay bin Ka’b anawasomea nao wanamfuata baada ya swalah yake.” Akasema: “Wamefanya vyema” (au: wamepatia).” Hakuchukizwa na kitendo chao.”

Ameipokea al-Bayhaqiy (2/495), ambaye amesema kuwa ”kuna swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi na ni nzuri”. Hata hivyo imepokelewa kwa cheni ya wapokezi ilioungana kupitia kwa Abu Hurayrah ambayo haina neno kwa lengo la ufuatiliaji na kutilia nguvu. Amepokea Ibn Naswr katika “Qiyaam-ul-Layl”, uk. 90. Abu Daawuud (1/217) na al-Bayhaqiy.

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 10
  • Imechapishwa: 10/02/2025