06- Wakati fulani alikuwa akiswali miguu peku na wakati mwingine akiswali na viatu[1].

Amewaruhusu hilo Ummah wake na kusema:

“Anaposwali mmoja wenu, ima avae viatu vyake au avivue na kuviweka kati ya miguu yake ili asimuudhi yeyote kwavyo.[2]

Amesisitiza ya kwamba mtu wakati mwingine aswali navyo na kusema:

“Jitofautisheni na mayahudi, kwani hakika wao haswali kwa viatu vyao wala soksi za ngozi.”[3]

Wakati mwingine alikuwa anaweza kuvivua ndani ya swalah na akaendelea na swalah yake. Abu Sa´iyd al-Khudriy amesema:

“Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituswalisha. Tahamaki katikati ya swalah akavivua na kuviweka upande wake wa kushoto. Watu walipomwona akifanya hivo, nao wakavua viatu vyao. Alipomaliza kuswali, akasema: “Ni kwa nini mmevua viatu vyenu?” Wakasema: “Tumekuona ukivua viatu vyako nasi tukavua viatu vyetu.” Akasema: “Jibriyl alinijia kunambia kuwa vina najisis (au alisema “uchafu”), (na katika upokezi mwingine “taka”) ndio nikawa nimevivua. Mmoja wenu anapokuja msikitini, atazame viatu vyake. Akiona vina najisi (au alisema “uchafu”), (na katika upokezi mwingine “taka”) aitoe kisha aswali navyo.”[4]

Alikuwa pindi anapovivua anaviweka upande wake wa kushoto[5].

Alikuwa vilevile akisema:

“Mmoja wenu anaposwali asiweke viatu vyake upande wa kulia wala wa kushoto vikawa upande wa kulia wa mwingine, isipokuwa ikiwa kama upande wake wa kushoto hakuna mtu. Aviweke kati ya miguu yake.”[6]

[1] Abuu Daawuud na Ibn Maajah. at-Twahaawiy ametaja kuwa Hadiyth hii imepokelewa kwa mapokezi mengi.

[2] Abuu Daawuud na al-Bazzaar (53) al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

[3] Abuu Daawuud na al-Bazzaar (53) al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

[4] Abuu Daawuud, Ibn Khuzaymah na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy na an-Nawawiy wameafikiana naye. Imetajwa vilevile katika ”al-Irwaa’”(284).

[5] Abuu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Khuzaymah (1/110/2) kwa isnadi Swahiyh.

[6] Abuu Daawuud, Ibn Khuzaymah na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy na an-Nawawiy wameafikiana naye.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 79-80
  • Imechapishwa: 13/10/2016