06. Kulingania katika dini ya Allaah ni lazima

1 – Ubainifu wa hukumu ya kulingania kwa Allaah na ubainifu wa fadhilah zake

Kuhusu hukumu yake ni kwamba dalili za Qur-aan na Sunnah zimejulisha juu ya ulazima wa kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba ni katika mambo ya lazima. Dalili juu yake ni nyingi ikiwa ni pamoja na maneno Yake (Subhaanah):

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚوَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Wawepo kutoka kwenu watu wanaolingania kheri na kuamrisha mema na unaokataza maovu. Hao ndio waliofaulu.”[1]

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[2]

وَادْعُ إِلَىٰ رَبِّكَ ۖ وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

”Na lingania kwa Mola wako na wala usiwe miongoni mwa washirikina.”[3]

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[4]

Akabainisha (Subhaanah) ya kwamba wafuasi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio wenye kulingania katika dini ya Allaah na wenye utambuzi. Kilicho cha lazima – kama inavyotambulika – ni kumfuata na kupita juu ya mfumo wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[5]

Wanazuoni wamesema wazi ya kwamba kulingania kwa Allaah ni faradhi kwa baadhi ya watu. Kila nchi na kila eneo linahitaji walinganizi nakuwepo na uchangamfu. Kwa hivyo ni faradhi kwa baadhi ya watu. Wakipatikana baadhi ya wenye kutosheleza basi uwajibu huo unaanguka kutoka kwa wengine. Ulinganizi kwa wale wengine itakuwa ni Sunnah iliyokokotezwa na kitendo kizuri na kitukufu.

Ikiwa watu wa eneo fulani au watu wa nchi fulani hawatosimamia kazi ya ulinganizi kwa njia kamilifu, basi dhambi zinawapata wote na ulazima unamgusa kila mmoja. Ni lazima kwa kila mtu kusimamia jambo la kulingania kwa kiasi cha uwezo wake. Ama tukitazama nchi nzima kwa ujumla wake ni lazima kuwepo kundi teule ambalo linasimamia kazi ya kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) ulimwenguni kote ambalo linafikisha ujumbe wa Allaah na kubainisha maamrisho ya Allaah (´Azza wa Jall) kwa njia zinazowezekana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatuma walinganizi, akawatumia barua watu, wafalme na maraisi na akawalingania kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Hii leo Allaah (´Azza wa Jall) amerahisisha jambo la ulinganizi kwa kiasi kikubwa kwa njia ambazo hazikuweko kwa waliokuwa kabla yetu. Mambo ya kulingania leo yamekuwa mepesi kwa kiasi kubwa kupitia njia nyingi. Hii leo watu wanaweza kubainishiwa hoja kwa njia mbalimbali kukiwemo redio, runinga na vyombo vya mawasiliano.

[1] 03:104

[2] 16:125

[3] 28:87

[4] 12:108

[5] 33:21

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 13-16
  • Imechapishwa: 31/05/2023