an-Nakha´iy alikuwa anaona hakuna neno mtu kusoma elimu ya nyota kwa lengo la kuongoka njia. Harb amenukuu kwamba Ahmad na Ishaaq wamejuzisha kusoma matuo ya mwezi. Ishaaq amesema pia:

“Inafaa kusoma elimu ya nyota kwa lengo la kuongoka njia.”

Qataadah amechukizwa kusoma matuo ya mwezi na Ibn ´Uyaynah hakuruhusu jambo hilo, ndivo alivosema Harb. Twawuus amesema:

“Pengine yule mwenye kusoma nyota na alfabeti hana mbele ya Allaah fungu.”

Ameipokea Harb. Humayd bin Zanjuuyah ameipokea kutoka kwa Twawuus kupitia kwa Ibn ´Abbaas. Haya yanalenga elimu ya kuathiri na sio elimu ya shughuli, kwani elimu ya kuathiri ni batili na haramu. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu ya jambo hilo:

“Yeyote atakayejifunza sehemu ya elimu ya nyota basi atakuwa amejifunza sehemu katika uchawi. Vile anavyojizidishia hujizidishia.”[1]

Qabiyswah ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuwashtua ndege wakaruka, kuchora msitari ardhini na kufanya mkosi juu ya ndege ni katika uchawi.”[2]

Kwa maana hiyo ni kwamba ni batili na haramu kuona kuwa nyota zinaathiri katika ulimwengu pamoja na kuziabudu na kuzitekelezea nadhiri. Hata hivyo kikosi cha wanazuoni wengi wanaona kuwa mtu akijifunza elimu ya shughuli kiasi ambacho anakihitajia ili apate kuongoka njia na kujua Qiblah kilipo ni kitu kinachofaa.

[1]Abu Daawuud (3905), Ibn Maajah (3726), Ahmad (2841) na al-Bayhaqiy (16290). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (11019).

[2]Abu Daawuud (3907), Ahmad (20623), at-Twabaraaniy (941) na al-Bayhaqiy (16292). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf-ul-Jaami´” (8336).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 44-47
  • Imechapishwa: 14/09/2021