Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

12 – Mwenye kufisha bila ya khofu yoyote, Mwenye kufufua bila ya uzito wowote.

13 – Ni Mwenye kusifika milele juu ya sifa Zake kabla ya kuumba Kwake.

14 – Sifa Zake hazikuongezeka kutokana nao.

15 – Kama ambavyo siku zote alikuwa ni mwenye kusifiwa kwa sifa Zake, vivyo hivyo ndivo atavoendelea kuwa milele.

16 – Hakuwa ni Muumbaji baada ya kuumba wala Mwanzilishi viumbe baada ya kuanzisha viumbe.

17 – Alikuwa na sifa ya uungu wakati hapakuwa yeyote wa kuabudu, alikuwa ni Muumbaji wakati hapakuwa kiumbe yeyote.

18 – Kama ambavyo anazingatiwa ni Mwenye kuwahuisha wafu na amestahiki jina hili kabla ya kuwapa uhai, kadhalika amestahiki jina la Muumbaji kabla ya kuwaumba.

19 – Kwa sababu Yeye juu ya kila jambo ni muweza. Kila kitu ni chenye kumuhitajia Yeye. Kila jambo Kwake ni jepesi:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

MAELEZO

Baadhi wanasema kuwa Allaah ni muweza kwa yale anayoyataka. Hayo si sahihi. Sahihi ni yale yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah; kwamba Yeye juu ya kila kitu ni muweza kwa sababu matakwa na uwezo Wake ni vyenye kuenea.

Mu´tazilah wanasema kuwa Allaah (Ta´ala) hakutaka mja aingie ndani ya madhambi; bali mja mwenyewe ndiye kataka hivo, na si Allaah. Kwa ajili hiyo amesema mmoja katika wapotofu wao:

Amedai mjinga na yule mwenye kuonelea kama yeye

ya kwamba Muumba ndiye kahukumu maasi

ikiwa hayo anayoyasema ni kweli

ni kwa nini basi aadhibiwe mzinzi na mwizi akatwe mkono?

Abul-Khattwaab (Rahimahu Allaah) amesema pindi alipokuwa akibainisha haki na usawa:

Wamesema: “Vipi basi matendo ya waja?”

Nikasema hakuna Muumba isipokuwa Mungu mtukufu

Wakasema: “Je, anataka kutokee kwa mambo mabaya?”

Nikasema matakwa yote yanayotokana na Mola

Ni upungufu ikiwa yatatokea pasi na kutaka Kwake

Ametakasika kushindwa na kitu duni

Matakwa anayozungumzia Abul-Khattwaab ni ya kilimwengu, na si ya kidini. Hayo yatakuja kubainishwa huko mbele.”[2]

[1] 42:11

[2] Haashiyah ´alaa al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 23-24

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 12/09/2024