Ndio maana nikasema tunatakiwa kutilia umuhimu kuutambua mfumo wa Salaf na kuusoma inapokuja katika ´Aqiydah, tabia na kuifanyia kazi katika nyanja zote. Salafiyyah ndio mfumo aliokuwemo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wale waliofuata uongofu wao na wakafata mfumo wao mpaka kisimame Qiyaamah.”

Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakitoacha kipote katika ummah wangu… “

Hawa ndo Salaf na Salafiyyuun.

“… kuwa juu ya haki na hali ya kuwa ni wenye kushinda. Hawatowadhuru wale wenye kuwakosesha nusura na wenye kwenda kinyume nao mpaka ifike amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”[1]

Maneno yake (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

“Hawatowadhuru wale wenye kuwakosesha nusura na wenye kwenda kinyume nao… “

Yanafahamisha kuwa kutakuwa wenye kwenda kinyume nao na wenye kuwatosa, lakini hata hivyo asiwajali. Yeye anafuata njia ya kumfikisha kwa Allaah (´Azza wa Jall) na wakati huohuo anastahamili yale yenye kumsibu. Luqmaan alimwambia mwanae hali ya kumpa mawaidha:

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ إِنَّ ذَلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ

“Ewe mwanangu! Simamisha swalah na amrisha mema na kataza maovu na subiri kwa yanayokupata, kwani hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika ardhi kwa maringo; hakika Allaah hampendi kila anayejivuna na kujifakhirisha. Na ushike mwendo wa katikati na shusha sauti yako; hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyozidi ni sauti ya punda.”[2]

Huu ndio mfumo wa Salaf. Hizi ndizo alama na sifa zao. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَأَنَّ هَـذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Hii ndio Njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni na wala msifuate njia zingine zitakufarikisheni na Njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kumcha Allaah.”[3]

Maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ هَـذَا صِرَاطِي

“Hii ndio Njia Yangu… “

Ameinasibisha Kwake Mwenyewe. Unasibishaji wa kujitukuza Yeye na yule mwenye kuifuata:

وَأَنَّ هَـذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ

“Hii ndio Njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni na wala msifuate njia zingine… ”

Ni dalili yenye kufahamisha kuwa kuna vijia vingine. Hakuviwekea kikomo. Ni vichochoro vingi.

وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ

”… na wala msifuate njia zingine zitakufarikisheni… ”

Huu ndio mfumo wa makundi yanayoenda kinyume na mfumo wa Salaf.

وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

”… na wala msifuate njia zingine zitakufarikisheni na Njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kumcha Allaah.”

Ameanza (Subhaanah) kwa kusema:

فَاتَّبِعُوهُ

“… basi ifuateni… “

Halafu akasema:

ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

”Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kumcha Allaah.”

Huenda kwa kufanya hivo mkamcha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kuogopa upotevu, hoja tata na kuogopa vizuizi vilivyoko katika kuifikia Njia hii. Ni dalili yenye kuonesha kuwa mtafikwa na mambo. Tazama namna Alivyoifanya Njia Yake kuwa moja na akafanya njia za vichochoro kuwa vingi. Njia ya Allaah iliyonyooka ni moja peke yake na sio nyingi. Kuhusiana na njia za vichochoro ni nyingi hazihesabiki. Kila mmoja amejichukulie njia na mfumo anaoufuata yeye na wafuasi zake. Kwa hivyo njia za vichochoro ni nyingi:

وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ

“… na wala msifuate njia zingine… “

Endapo mtafanya hivyo kutatokea nini?

فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

”… zitakufarikisheni na Njia Yake.”

Zitakutoeni katika Njia ya Allaah (´Azza wa Jall). Mtatumbukia ndani ya upotofu na maangamivu. Hivyo hakuna uokovu, wema na mafanikio isipokuwa kwa kulazimiana na Njia iliyonyooka. Hiyo ndio Njia ya Allaah (´Azza wa Jall). Kila njia nyingine yenye kwenda kinyume nayo ni njia ya shaytwaan. Katika kila njia hiyo kuna shaytwaan anayelingania watu kwayo. Tutahadhari na jambo hili. Tusidanganyike na kubabaika na wingi wa wapinzani na hoja zao tata. Usijali! Tufuate Njia ya Allaah kwa ujuzi.

[1] al-Bukhaariy (3640), (7311), (7459) na Muslim (1921).

[2] 31:17-19

[3] 06:153

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: as-Salafiyyah haqiyqatuhaa wa simaatuhaa, uk. 20-25