Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Sha´baan inapofika katikati, basi msifunge…”

Maana ya dhahiri ya Hadiyth hii inaonekana kupingana na Hadiyth ya mlango huu, kwa sababu Hadiyth ya mlango huu inakataza kufunga siku moja au mbili kabla ya kuanza Ramadhaan. Kinachopata kufahamika ni kwamba inajuzu kufunga kabla ya hapo.  Hata hivyo Hadiyth hii inakataza kufunga kuanzia katikati ya Sha´baan. Hadiyth hii kuna maoni tofauti juu ya kusihi kwake, kama itakavyoelezwa baadaye. Lakini tukikadiria kuwa ni Swahiyh basi maana yake ni kwa yule anayefunga swawm inayopendeza kuanzia katikati ya Sha´baan. Hata hivyo wale walio na desturi ya kufunga jumatatu na alkhamisi, au kufunga siku moja na kufungua nyingine, wale wanaoendelea kufunga Sha´baan baada ya nusu yake au wale walio na deni la swawm, basi hawaingii ndani ya katazo hili, kama ilivyotangulia kusemwa. at-Twahaawiy ametaja uwezekano mwingine; akisema kwamba Hadiyth hii inahusu wale ambao kufunga kutawadhoofisha kufunga kwa namna ya kwamba udhaifu huo utawaathiri kufunga Ramadhaan. Hadiyth ya mlango huu inahusiana na wale wanaofunga kwa madai ya kuchukua tahadhari kwa ajili ya Ramadhaan[1]. Maneno yake yamenukuliwa na Haafidhw na akasema kuwa ni uoanishaji mzuri[2] – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] Sharh Ma´aaniy-il-Aathaar (6/84-85)).

[2] Fat-ul-Baariy (4/169)).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/08)
  • Imechapishwa: 29/01/2025