2 – Jambo la pili ambalo kwa hilo moyo husimama sawa ni kutukuza amri na makatazo. Hili linatokana na kumtukuza Mwenye kuamrisha na kukataza. Hakika Allaah (Ta´ala) amewasimanga wale wasiomtukuza Yeye katika amri na makatazo. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

مَّا لَكُمْ لَا تَرْجُونَ لِلَّـهِ وَقَارًا

”Mna nini? Hamtaraji na hamkhofu Taadhima ya Allaah?”[1]

Wakasema wafasiri wa Qur-aan kwamba ni kwa nini hamumuogopi Allaah (Ta´ala) utukufu wa Allaah. Ni uzuri uliyoje wa yale aliyosema Shaykh-ul-Islaam katika kufasiri kutukuza kwa amri na katazo:

“Ni kwamba yasipingwe kwa ruhusa za uzembe, yasikabiliwe kwa misimamo ya kupindukia wala yasibebeshwe kwa hoja zinazodhoofisha utii.”[2]

Maana ya maneno yake ni kwamba daraja ya kwanza kabisa ya kumtukuza wa Haki (´Azza wa Jall) ni kutukuza amri Zake na makatazo Yake. Muumini humjua Mola wake (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa njia ya ujumbe aliomletea Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa watu wote na matokeo yake ni kunyenyekea kwa amri na katazo hilo. Jambo hilo linapatikana kwa kuyatukuza maamrisho ya Allaah kwa kuyafuata na kuyatukuza makatazo Yake kwa kuyaepuka. Basi kutukuza muumini kwa amri na katazo la Allaah ni dalili ya kumtukuza kwake Yeye mwenye kuamrisha na kukataza. Kwa kadri ya kutukuza huku mtu huwa miongoni mwa wema waliothibitishiwa imani, uaminifu, usahihi wa ´Aqiydah na kujitenga na unafiki mkubwa.

Wakati mwingine mtu anaweza kufanya amri kwa ajili ya macho ya watu na kutafuta hadhi na nafasi mbele yao, au akaepuka makatazo kwa kuogopa kuanguka machoni mwa watu, kwa kuogopa adhabu za kidunia kama zile adhabu za kidini zilizowekwa na Shari´ah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya makatazo. Huyu kutenda kwake na kuacha kwake hakukutokana na kutukuza amri na katazo wala kwa kumtukuza Yule mwenye kuamrisha na kukataza.

[1] 71:13

[2] Manaazil-us-Saa-iriyn (65) ya al-Harawiy.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 28/07/2025