05. Baadhi ya faida za swalah ya mkusanyiko na tahadhari kujifananisha na wanafiki

Haifichikani kuswali kwa mkusanyiko kuna faida nyingi na manufaa makubwa. Miongoni mwa manufaa yaliyo wazi zaidi ni kujuana na kusaidiana katika wema na uchaji Allaah, kushauriana kwa haki na kusubiri juu yake, kumuhimiza anayebakibaki nyuma, kumfunza mjinga, kuwakasirisha wanafiki, kujiepusha na mwenendo wao, kudhihirisha nembo ya Allaah kati ya waja Wake, kulingania katika dini ya Allaah kwa maneno na vitendo na faida nyenginezo ambazo ni nyingi.

Miongoni mwa watu wako ambao wanaweza kukesha usiku na wakachelewa kuswali Fajr. Baadhi ya wengine wakaacha kuswali ´Ishaa. Hapana shaka kwamba hayo ni maovu makubwa na ni kujifananisha na maadui wa dini wanafiki ambao Allaah (Subhaanah) amesema juu yao:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَن تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto na wala hutompata kwa ajili yao mwenye kunusuru.”[1]

Amesema tena (´Azza wa Jall) juu yao:

الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُم مِّن بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمُنكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ وَيَقْبِضُونَ أَيْدِيَهُمْ ۚ نَسُوا اللَّـهَ فَنَسِيَهُمْ ۗ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake wenyewe kwa wenyewe, wanaamrisha maovu na wanakataza mema na hufumba mikono yao; wamemsahau Allaah, basi Naye amewasahau. Hakika wanafiki wao ndio mafasiki.”[2]

وَعَدَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْكُفَّارَ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ هِيَ حَسْبُهُمْ ۚ وَلَعَنَهُمُ اللَّـهُ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ

”Allaah amewaahidi wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri Moto wa Jahannam hali ya kuwa ni wenye kudumu humo – unawatosheleza – na Allaah amewalaani na watapata adhabu ya milele.”[3]

وَمَا مَنَعَهُمْ أَن تُقْبَلَ مِنْهُمْ نَفَقَاتُهُمْ إِلَّا أَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَبِرَسُولِهِ وَلَا يَأْتُونَ الصَّلَاةَ إِلَّا وَهُمْ كُسَالَىٰ وَلَا يُنفِقُونَ إِلَّا وَهُمْ كَارِهُونَ فَلَا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُمْ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُعَذِّبَهُم بِهَا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ

”Haikuwazuilia kukubaliwa michango yao isipokuwa kwa kuwa wao walimkufuru Allaah na Mtume Wake na wala hawaiendei swalah isipokuwa wao huwa katika hali ya uvivu na wala hawatoi isipokuwa wakiwa wamechukia. Basi zisikupendezee mali zao na wala wana wao. Hakika Allaah anataka kuwaadhibu kwayo katika uhai wa dunia na zitoke nafsi zao na huku wao wakiwa makafiri.”[4]

Kwa hivyo ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na muislamu wa kike kutahadhari na kujifananisha na wanafiki hawa katika matendo na maneno yao na kuhisi kwao uzito wa swalah na kuacha kwao kuswali Fajr na ´Ishaa ili asije kufufuliwa pamoja nao. Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Swalah nzito kwa wanafiki ni swalah ya ´Ishaa na swalah ya Fajr. Endapo wangelijua yanayopatikana ndani yake basi wangeziendea ijapo ni kwa kutambaa.”[5]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao.”[6]

Ameipokea Imaam Ahmad kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwa cheni ya wapokezi nzuri.

[1] 04:145

[2] 09:67

[3] 09:68

[4] 09:54-55

[5] al-Bukhaariy (617) na Muslim (1041).

[6] Abu Daawuud (3512) na Ahmad (4868).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 16/11/2021