05. Anayofaa mwanamke kuonyesha kwa mtazamo wa al-Qurtwubiy

Naona kuwa kuipa nguvu huku kuna nguvu kwa sababu sio kitu ambacho kinafahamika haraka katika Aayah. Bali utiwaji nguvu huo ni wa inavopelekea jambo ambalo halipelekei hivo kwa hapa. Kwa sababu mpinzani anaweza kusema kuwa kufaa kwa mwanamke kuonyesha uso wake ndani ya swalah ni jambo malaum ndani ya swalah peke yake, lakini si pale anapotoka nje ya swalah kwa sababu ya kutofautiana waziwazi kati ya hali hizo mbili.

Nayasema haya licha ya kwamba nakubaliana naye kwamba inafaa kwake kuonyesha uso wake, mikono yake na viganja vya mikono wakati anaposwali na nje yake. Zipo dalili nyingi mbali na hii. Lakini hapa tunachojadili ni kusihi kwa dalili hii, na si kusihi kwa madai haya. Haki juu ya maana ya ubaguaji huu ni yale tuliyotanguilia kuyataja na tukayatilia nguvu kwa maneno ya Ibn Kathiyr. Yanatiliwa nguvu zaidi na maneno ya al-Qurtwubiy:

”Ibn ´Atwiyyah amesema: ”Kinachonidhihirikia kutokana na tamko la Aayah ni kwamba mwanamke ameamrishwa asionyeshe na ajitahidi kufunika kila ambacho ni mapambo isipokuwa kile ambacho amelazimika kionekane wakati wa matikiso ambayo hayaepukiki, haja na mfano wake. Maneno:

إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“… isipokuwa yale yanayodhihirika… “[1]

ni kuhusu yale ambayo wanawake wamedharurika kwayo. Ni mwenye kusamehewa kwayo.”

al-Qurtwubiy amesema:

”Haya ni maneno mazuri. Lakini ilipokuwa mara nyingi kuonekana kwa uso na mikono ni jambo la kawaida na katika ´ibaadah, kama vile ndani ya swalah na hajj, hivyo ni sawa ikawa ubaguliwaji unarejea katika viwili hivyo. Yanafahamisha hivo ile Hadiyth aliyoipokea Abu Daawuud kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

”Wakati ´Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alipoingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa amevaa nguo nyembamba, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akageuka na kumwambia: ”Ee Asmaa´! Hakika mwanamke anapobaleghe basi haifai kwake kuonyesha kitu isipokuwa haya” na akaashiria uso na mikono yake.”

Hili ni lenye nguvu zaidi kwa upande wa kuchukua tahadhari zaidi, lakini na kwa kuchunga kutoharibika kwa watu. Kwa hivyo haitakiwi kwa mwanamke kuonyesha mapambo yake isipokuwa yale yanayodhihiri katika uso na mikono yake.”

[1] Jaamiy´ li Ahkaam-il-Qur-aan (12/229).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 50-51
  • Imechapishwa: 30/08/2023