Tawhiyd imegawanyika aina mbili:

1- Tawhiyd fiyl-Ma´rifah wal-Ithbaat. Nayo ni Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Mifano yake ni kukubali uumbaji, kupwekeka Kwake juu ya kuumba, kuyaendesha mambo, kuhuisha, kufisha, kuleta kheri na kuzuia shari. Aina hii anakaribia kutokuwepo kiumbe yeyote anayeipinga. Mpaka washirikina licha ya shirki zao walikuwa wakiikubali. Kama alivyosema Allaah (Ta´ala) katika maneno Yake:

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu na anayemtoa mfu kutoka aliye hai na nani anayeendesha mambo?”  Watasema: “Ni Allaah”, basi sema: “Je, basi kwa nini hamchi?”[1]

Mfano wa Aayah kama hizi ni nyingi. Ndani yake kuna mabainisho ya wazi ya kwamba washirikina walikuwa wakiikubali aina hii ya Tawhiyd. Walichokuwa wakipinga ni aina ya pili ya Tawhiyd:

2- Tawhiyd-ul-´Ibaadah. Ni kule kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) katika maombi katika kila aina ya ´ibaadah anayofanya mja. Hivyo ndivyo inavofahamisha neno “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Neno hili linamthibitishia Allaah pekee aina zote za ´ibaadah na kumkanushia mwengine asiyekuwa Yeye. Kwa ajili hiyo wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowataka washirikina walitamke walikataa na wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!”[2]

Kwa sababu walijua kwamba yule mwenye kulitamka amejikubalisha mwenyewe ubatilifu wa kumtekelezea ´ibaadah mwingine asiyekuwa Allaah na badala yake kumthibitishia ´ibaadah Allaah pekee. Kwani الإله mungu maana yake ni المعبود mwabudiwa.

´Ibaadah ni neno lililokusanya matendo na maneno yote anayoyapenda Allaah na kuyaridhia. Ni sawa maneno hayo yakawa ya waziwazi au yaliyojificha.

Mwenye kutamka neno hili na wakati huohuo akawa anaomba wengine pamoja na Allaah amejigonga mwenyewe.

Mafungamano kati ya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na Tawhiyd-ul-Ilaahiyyah ni yenye kwenda sambamba. Kwa msemo mwingine ni kwamba kukubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah kunapelekea mtu kukubali Tawhiyd-ul-Ilaahiyyah na kuitendea kazi kwa uinje na kwa undani. Ndio maana Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walikuwa wakiwataka nyumati zao kufanya hivo na wakitumia hoja dhidi yao kutokana na ile Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah waliokuwa wanakubali. Amesema (Ta´ala):

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ فَاعْبُدُوهُ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ

“Huyo ndiye Allaah, Mola wenu. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Muumbaji wa kila kitu, hivyo basi mwabuduni Yeye pekee. Naye juu ya kila kitu ni mdhamini anayetegemewa kwa yote.”[3]

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۚ قُلْ أَفَرَأَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَنِيَ اللَّـهُ بِضُرٍّ هَلْ هُنَّ كَاشِفَاتُ ضُرِّهِ أَوْ أَرَادَنِي بِرَحْمَةٍ هَلْ هُنَّ مُمْسِكَاتُ رَحْمَتِهِ

“Ukiwauliza: “Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi?” Bila shaka watasema: “Allaah.” Sema: “Je, mnaonaje wale mnaowaomba badala ya Allaah ikiwa Allaah atanikusudia dhara, je, wao wataweza kunidoshea dhara Yake au akinikusudia rehema, je, wao wataweza kuniondoshea rehema Yake?”[4]

Kukubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ni jambo limekita kwenye maumbile. Anakaribia kutokuwepo yeyote anayezozana juu ya hili. Haijulikani kama kuna yeyote katika makundi ya ulimwengu ambaye anapinga aina hii isipokuwa Dahriyyah ambao wanamkanusha Muumba na wanadai kuwa ulimwengu unajiendesha wenyewe pasi na mwenye kuuendesha. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu wao:

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ

“Wakasema: “Haya si chochote isipokuwa ni uhai wetu wa dunia, tunakufa na tunahuika, na hakuna cha kutuangamiza isipokuwa zama tu.”[5]

Ndipo Allaah akawaraddi kwa kusema:

وَمَا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ

“Na wala hawana kwayo ujuzi wowote, si vyenginevyo wao wanadhania tu.”[6]

Hawakujenga makanusho yao haya juu ya hoja. Bali wameyajenga juu ya dhana tupu. Dhana haisaidii kitu katika haki. Kama ambavyo wao hawakuweza kujibu maneno Yake (Ta´ala):

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ  أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.”[7]

هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ

”Huu ni uumbaji wa Allaah, basi nionyesheni ni kitu gani walichokiumba wasiokuwa Yeye.”[8]

قُلْ أَرَأَيْتُمْ شُرَكَاءَكُمُ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَرُونِي مَاذَا خَلَقُوا مِنَ الْأَرْضِ أَمْ لَهُمْ شِرْكٌ فِي السَّمَاوَاتِ

”Sema: “Je, mnawaona washirika wenu ambao mnawaomba badala ya Allaah – nionyesheni ni nini walichoumba katika ardhi au wana ushirika wowote ule mbinguni?”[9]

Yule atayejionyesha kupinga aina ya Tawhiyd hii kwa uinje, kama alivofanya Fir´awn, basi ni mwenye kuikubali kwa ndani. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Fir´awn:

قَالَ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا أَنزَلَ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ

“Akasema: “Hakika umekwishajua kwamba hakuna aliyeteremsha haya isipokuwa Mola wa mbinguni na ardhini.”[10]

Vilevile akasema kuhusu yeye na watu wake:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا

“Wakazipinga kwa dhuluma na majivuno na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha. “[11]

Amesema (Ta´ala) kuhusu nyumati za hapo kale:

وَعَادًا وَثَمُودَ وَقَد تَّبَيَّنَ لَكُم مِّن مَّسَاكِنِهِمْ ۖ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَكَانُوا مُسْتَبْصِرِينَ

“Kina ‘Aad na Thamuud na bila shaka  [maangamizi yao] yamekwishakubainikieni katika masikani zao na shaytwaan aliwapambia matendo yao akawazuia na njia, japokuwa walikuwa ni wenye kutambua vyema.”[12]

[1] 10:31

[2] 38:05

[3] 06:102

[4] 39:38

[5] 45:24

[6] 45:23

[7] 52:35-36

[8] 31:11

[9] 35:40

[10] 17:102

[11] 27:14

[12] 29:38

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 09-14
  • Imechapishwa: 21/03/2019