04- Akiwa na haki za wenyewe basi azisalimishe kwa wenyewe ikimsahilikia kufanya hivo. Vinginevyo aache anausia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote ambaye atakuwa na alichomdhulumu ndugu yake – heshima au mali yake – basi amrudishie kabla haijamfikia yeye siku ya Qiyaamah ambapo hakutokubaliwa dinari wala dirhamu. Akiwa na matendo mema yatachukuliwa kutoka kwake na apewe mwenzake. Akiwa hana matendo mema, basi yatachukuliwa maovu ya mwenzake na apewe yeye.”

Ameipokea al-Bukhaariy, al-Bayhaqiy (03/369) na wengineo.

Amesema vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hivi mnajua ni nani aliyefilisika?” Wakasema: “Aliyefilisika kwetu ni yule asiyekuwa na pesa wala kitegauchumi.” Akasema: “Aliyefilisika katika Ummah wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyaamah akiwa na swalah, swawm na zakaah. Lakini amemtukana huyu, amemtuhumu machafu yule, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya yule na amempiga yule. Atapewa huyu kutoka katika matendo yake mema na mwingine  kutoka katika matendo yake mema. Matendo yake mema yakiisha kabla yeye kuhukumiwa, basi yatachukuliwa madhambi na makosa yao atwishwe nayo kisha atupwe Motoni.”

Ameipokea Muslim (08/18).

Amesema pia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayekufa ilihali yuko na deni [basi alilipe upesi], kwani [huko Aakhirah] hakuna dinari wala dirhamu. Lakini matendo mema na maovu.”

Ameipokea al-Haakim (02/27) na siyaaq ni yake, Ibn Maajah, Ahmad (02/70-82) kupitia njia mbili kutoka kwa Ibn ´Umar. Njia ya kwanza ni Swahiyh kama alivyosema al-Haakim na adh-Dhahabiy akaafikiana naye na njia yake ya pili ni nzuri kama alivosema al-Mundhiriy (03/34). at-Twabaraaniy ameipokea katika “al-Kabiyr” kwa tamko lisemalo:

“Madeni yako aina mbili. Mwenye kufa ilihali alikuwa amenuia kulipa deni lake, basi mimi ndiye msimamizi wake. Na mwenye kufa ilihali hakuwa amenuia kulipa deni lake, huyo ndiye ambaye yatachukuliwa matendo yake mema siku ambayo hakutokuwa na dinari wala dirhamu.”[1]

Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Wakati ilipofika vita vya Uhud, baba yangu aliniita kipindi cha usiku na akanambia: “Mimi sioni isipokuwa nitakuwa miongoni mwa watakaouliwa mwanzoni katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mimi hakuna mwingine nitakayemwacha nyuma yangu ambaye ni mwenye thamani zaidi kwangu – mbali na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – kuliko wewe. Mimi nina deni na hivyo nilipie. Kuwa sababu ya kheri kwa ndugu zako. Tukapambaukiwa na asubuhi na hivyo akawa miongon mwa wa mwanzo waliouawa… “

Ameipokea al-Bukhaariy (1351).

05- Ni wajibu kuharakisha wasia kama huu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si haki kwa muislamu kulala nyusiku mbili ilihali yuko na kitu ambacho anataka kuusia isipokuwa wasia wake uwe umeandikwa chini ya mto wake.”

Ibn ´Umar amesema:

“Tangu nimsikie Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema hivo hakujawahi kupita usiku wowote isipokuwa nimeandika wasia wangu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim, waandishi wa “as-Sunan” na wengineo.

06- Ni wajibu kutoa wasia wenye kuwahusu ndugu zake wa karibu ambao hawamrithi. Amesema (Tabaarak wa Ta´ala):

كُتِبَ عَلَيْكُمْ إِذَا حَضَرَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ إِن تَرَكَ خَيْرًا الْوَصِيَّةُ لِلْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ

“Mmeandikiwa [shariy’ah] kuwa anapofikiwa mmoja wenu na mauti kama ameacha mali, kufanya wasia kwa wazazi wawili, na jamaa wa karibu kwa wema [namna inayoeleweka katika [shariy’ah]. Haya ni wajibu kwa wenye kumcha Allaah.”[2]

07- Inafaa kuacha anausia theluthi ya mali yake na wala haijuzu kuzidisha hapo. Bali lililo bora ni kupunguza kiwango hicho kutokana na Hadiyth ya Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Nilikuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj ya kuaga. Nikauguwa maradhi ambayo nilikaribia kufa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja kunitembelea ambapo nikasema: “Ee Mtume wa Allaah!  Hakika mimi nina mali nyingi na sina wenye kunirithi zaidi ya msichana wangu. Je, inafaa kwangu kuusia sehemu mbili ya theluthi zangu?” Akasema: “Hapana.” Nikasema: “Nusu ya mali yangu?” Akasema: “Hapana.” Nikasema: “Theluthi moja ya mali yangu.” Akasema: “Theluthi ni sawa, hata hivyo theluthi ni nyingi. Ee Sa´d! Hakika kuwaacha warithi wako ni matajiri ni bora kwako kuliko kuwaacha masikini wakiwaombaomba watu [akaashiria kwa mkono wake]. Ee Sa´d! Hakika hutotoa matumizi yoyote ukitafuta kwayo uso wa Allaah (Ta´ala) isipokuwa utapewa ujira kwayo mpaka tonge unalotia mdomoni mwa mke wako.”

[Anaendelea kusimulia:

“Ikawa baada ya theluthi inajuzu.”]

Ameipokea Ahmad (1524) na siyaaq ni yake, al-Bukhaariy na Muslim na nyongeza mbili ni za Muslim na waandishi wa “as-Sunan”.

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Ninapendelea kama watu watashuka kutoka kwenye theluthi kwenda chini katika robo wakati wa kutoa wasia. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Theluthi ni nyingi.”

Ameipokea Ahmad (2029,2076), al-Bukhaariy na Muslim na al-Bayhaqiy (06/269) na wengineo.

8- Ashuhudishe juu ya hilo wanaume wawili waadilifu ambao ni waislamu. Asipopata ni sawa akawashuhudisha wanaume wawili wasiokuwa waislamu kwa sharti iwe inawezekana kuchukuliwa ithbati pindi watu watapokuwa na mashaka kwa ushuhuda wao kutokana na vile ubainifu wake ulivyokuja katika maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

يَاأَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا شَهَادَةُ بَيْنِكُمْ إِذَا حَضَرَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ حِينَ الْوَصِيَّةِ اثْنَانِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ أَوْ آخَرَانِ مِنْ غَيْرِكُمْ إِنْ أَنتُمْ ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَأَصَابَتْكُم مُّصِيبَةُ الْمَوْتِ ۚ تَحْبِسُونَهُمَا مِن بَعْدِ الصَّلَاةِ فَيُقْسِمَانِ بِاللَّـهِ إِنِ ارْتَبْتُمْ لَا نَشْتَرِي بِهِ ثَمَنًا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۙ وَلَا نَكْتُمُ شَهَادَةَ اللَّـهِ إِنَّا إِذًا لَّمِنَ الْآثِمِينَ فَإِنْ عُثِرَ عَلَىٰ أَنَّهُمَا اسْتَحَقَّا إِثْمًا فَآخَرَانِ يَقُومَانِ مَقَامَهُمَا مِنَ الَّذِينَ اسْتَحَقَّ عَلَيْهِمُ الْأَوْلَيَانِ فَيُقْسِمَانِ بِاللَّـهِ لَشَهَادَتُنَا أَحَقُّ مِن شَهَادَتِهِمَا وَمَا اعْتَدَيْنَا إِنَّا إِذًا لَّمِنَ الظَّالِمِينَ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يَأْتُوا بِالشَّهَادَةِ عَلَىٰ وَجْهِهَا أَوْ يَخَافُوا أَن تُرَدَّ أَيْمَانٌ بَعْدَ أَيْمَانِهِمْ ۗ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاسْمَعُوا ۗ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ

“Enyi walioamini! Mauti yanapomfikia mmoja wenu wakati anapousia, basi chukueni ushahidi wa wawili wenye uadilifu miongoni mwenu au wawili wengineo wasiokuwa nyinyi pale mnapokuwa safarini ukakufikeni msiba wa mauti. Muwazuie baada ya swalah na waape kwa Allaah mkitilia shaka [waseme]: “Hatutovibadilisha [viapo vyetu] kwa thamani yoyote ile japo akiwa ni jamaa yetu wa karibu na wala hatutoficha ushuhuda wa Allaah, kwani hakika hapo tutakuwa miongoni mwa wenye kutenda dhambi. Ikigundilikana kwamba hao wawili wana hatia ya dhambi, basi wawili wengine wasimame mahali pao, wanaostahiki kudai haki Kishari´ah, walio karibu zaidi [na mrithiwa] kisha waape kwa Allaah: “Bila shaka ushahidi wetu ni wa kweli zaidi kuliko ushahidi wa wawili wao, nasi hatukufanya upetukaji; kwani bila shaka hapo sisi tutakuwa miongoni mwa madhalimu. Hivyo inaelekea zaidi ya kwamba watatoa ushahidi kama ipasavyo au watakhofu visije vikaletwa viapo vingine baada ya viapo vyao. Mcheni Allaah na sikizeni! Na Allaah hawaongozi watu mafasiki.”[3]

09- Kuhusu kuacha wasia juu ya wazazi wawili na ndugu wa karibu ambao wana haki ya kumrithi haifai. Kwa sababu ni jambo limefutwa kutokana na Aayah ya mirathi na akalibainisha hilo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ipasavyo katika Khutbah yake ya kuaga pale aliposema:

“Hakika Allaah amempa kila mwenye haki haki yake. Hivyo asiusiwe mwenye kurithi.”

Ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy ambaye ameifanya kuwa nzuri, al-Bayhaqiy (06/264) na akaashiria juu ya kuwa kwake na nguvu na amepatia. Kwani cheni yake ni nzuri. Kuna njia nyingi zenye kuisapoti kwa al-Bayhaqiy. Tazama “Majma´-uz-Zawaa-id” (04/212).

10- Imeharamishwa kuleta madhara katika wasia. Kwa mfano mtu akaacha anausia wanyimwe haki yao baadhi ya warithi au akawafadhilisha baadhi juu ya wengine. Amesema (Tabaarak wa Ta´ala):

لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ مِمَّا قَلَّ مِنْهُ أَوْ كَثُرَ ۚ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا

“Wanaume wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu na wanawake wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu, ikiwa ni kidogo au kingi, ni mgao uliofaridhishwa.”

Mwishoni mwake:

مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصَىٰ بِهَا أَوْ دَيْنٍ غَيْرَ مُضَارٍّ ۚ وَصِيَّةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَلِيمٌ

”Baada ya kutoa wasia uliousiwa na kulipwa deni pasipo kuleta dhara.  Huu ni wasia kutoka kwa Allaah, na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mvumilivu.”[4]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna kudhuriana. Mwenye kudhuru basi Allaah atamdhuru. Mwenye kusababisha mazito basi Allaah naye atampa mazito.”

Ameipokea ad-Daaraqutwniy (522), al-Haakim (02/57-58) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudhriy, adh-Dhahabiy ameafikiana naye, al-Haakim amesema:

“Swahiyh juu ya masharti ya Muslim.”

Haki ni kwamba ni Hadiyth nzuri kama alivosema an-Nawawiy katika “al-Arba´iyn”, Ibn Taymiyyah katika “al-Fataawaa” (03/262) kutokana na njia zake na shawahidi zake nyingi. Ameitaja vilevile Haafidhw Ibn Rajab katika “Sharh al-Arba´iyn”, uk. 219-220 kisha nikaipokea kwa upambanuzi zaidi katika “al-Irwaa´-ul-Ghaliyl” (888).

11- Wasia wenye dhuluma ni batili na ni wenye kurudishwa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kuzua katika dini yetu hii yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim katika “as-Swahiyh” zao, Ahmad na wengineo.

Vilevile kutokana na Hadiyth ya ´Imraan bin Huswayn aliyesimulia:

“Kuna mtu aliwaacha huru wakati wa kufa kwake watumwa sita. [Hakuwa na mali nyingine zaidi ya hii.] Wakaja warithi wake katika mabedui ambapo wakamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kile alichokifanya. Hivi kweli amethubutu kufanya hivo? Akasema: “Lau tungelijua basi tusingelimswalia – Allaah akitaka.” Akapiga kura kati yao ambapo akawaacha huru wawili na akawarudisha wanne katika utumwa.”

Ameipokea Ahmad (04/443), Muslim amepokea mfano wake, kadhalika at-Twahaawiy, al-Bayhaqiy na wengineo. Nyongeza ni ya Muslim na Ahmad katika upokezi mmoja.

[1] Ni Hadiyth Swahiyh kutokana na zile za kabla yake na kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah itayokuja huko mbele katika masuala ya 17.

[2] 02:180

[3] 05:106-108

[4] 04:12

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 04-08
  • Imechapishwa: 18/12/2019